• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:57 PM
Austria, Denmark zavunja uhusiano kuhusu chanjo ya corona

Austria, Denmark zavunja uhusiano kuhusu chanjo ya corona

Na MARY WANGARI

BRUSSELS, Ubelgiji

AUSTRIA na Denmark, zilivunja uhusiano wake na Brussels mnamo Jumanne, Machi 2, 2021, huku zikilalamikia kujikokota kwa usambazaji wa chanjo za COVID-19.

Nchi hizo zimeungana na Israeli kuunda chanjo za kizazi cha pili dhidi ya aina mpya ya virusi vya corona.

Hatua hiyo kutoka kwa mataifa hayo mawili ambayo ni wanachama wa Muungano wa Uropa, EU, imejiri huku hasira ikizidi kupanda kuhusu kucheleweshwa kwa uagiziaji, uidhinishaji na usambazaji wa chanjo.

Hali hiyo imefanya muungano huo wenye wanachama 27 kushikilia mkia kwa mbali katika kampeni kali za Israeli za usambazaji chanjo.

Rais wa Austria, Sebastian Kurz, alisema japo kanuni kwamba EU inapaswa kununulia chanjo mataifa wanachama wake ni sawa, Shirika la Dawa Uropa (EMA) limekuwa likijikokota mno kuwaidhinisha.

Alikashifu masharti tata kuhusu usambazaji wa dawa kutoka kwa mashirika ya dawa.

“Ni sharti tujiandae hivyo basi kwa aina nyinginezo za virusi na hatuwezi kutegemea EU pekee kwa uundaji wa chanjo za kizazi kipya,” alisema kiongozi huyo kupitia taarifa.

Waziri Mkuu nchini Denmark Mette Frederiksen vilevile alikosoa mpango wa EU kuhusu utowaji chanjo.

“Sidhani unaweza kujisimamia kivyake kwa sababu tunahitaji kuongeza uzalishaji. Ndiposa sasa tuna bahati ya kuanzisha ushirikiano na Israeli,” alieleza vyombo vya habari.

Alipoulizwa ikiwa Denmark na Austria zinataka kuchukua hatua ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kupata chanjo hizo Frederiksen: “unaweza kuiita hivyo.”

Kurz na Frederiksen wanatazamiwa kusafiri Israeli wiki hii kushuhudia kwa karibu uzinduzi wa kasi kuhusu chanjo nchini Israeli.

Kurz alisema Austria na Denmark, kama wanachama wa Kundi la Kwanza la Usogezaji, zitafanya kazi na Israeli kuhusu uundaji wa chanjo dhidi ya aina mpya ya virusi vya corona na kutafiti kwa pamoja kuhusu aina mbadala za tiba.

Wataalam wanafikiri kuwa Austria itahitajika kuwapa chanjo thuluthi mbili ya raia wake ambayo ni sawa na watu milioni sita, kila mwaka katika miaka ijayo, alifafanua Kurz.

Alisema atakagua kampuni za dawa zenye uzalishaji wa ndani ikiwemo Pfizer, Novartis. Polymun na Boehringer Ingelheim.

You can share this post!

Tunatoa huduma muhimu, tupewe chanjo ya corona, wasema...

Salman taabani kuhusu mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi