• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Biden ampa Trump kichapo cha mwisho kura za useneta

Biden ampa Trump kichapo cha mwisho kura za useneta

Na MASHIRIKA

ATLANTA, Amerika

RAIS Donald Trump wa Amerika jana Jumatano alipata kichapo cha mwisho cha kisiasa kutoka kwa Rais-Mteule Joe Biden, baada ya chama cha Democratic kupata ushindi mkubwa kwenye duru ya pili ya chaguzi mbili za useneta katika Jimbo la Georgia.

Kwenye uchaguzi wa kwanza, Kasisi Raphael Warnock wa Democratic aliibuka mshindi dhidi ya Kelly Loeffler, aliyewania nafasi hiyo kwa tiketi ya chama cha Republican, chake Trump.

Kulingana na asilimia 98 ya kura zilizokuwa zimehesabiwa kufikia Jumatano, Warnock alikuwa akiongoza kwa kuzoa asilimia 50.5 ya kura dhidi ya Loeffler, aliyekuwa amepata asilimia 49.5. Kwa sasa ana asilimia 50.8 huku Loeffler akiwa na asilimia 49.2.

Matokeo ya mwanzo kwenye uchaguzi wa pili kati ya John Ossoff wa Democratic na mwenzake David Perdue wa Republican, pia yalionyesha Democratic ilikuwa kifua mbele.

Wadadisi wa siasa wanasema kufuatia ushindi huo, chama cha Democratic sasa kitachukua udhibiti wa Bunge la Seneti, hali itakayompa Biden nafasi nzuri ya kuendeleza ajenda zake baada ya kuapishwa kuwa rais hapo Januari 20.

Warnock, 51, anahudumu kama mhubiri katika Kanisa la Ebenezer Baptist, jijini Atlanta.

Kanisa hilo ndiko alikokuwa akishiriki mwanaharakati Martin Luther King. Ushindi huo pia unamfanya kuwa Seneta wa kwanza Mweusi kuchaguliwa katika jimbo hilo.

“Nitaenda Seneti kuwafanyia kazi raia wote wa Georgia bila ubaguzi wala mapendeleo,” akasema Jumatano asubuhi, kwenye hotuba aliyotoa kwa njia ya mtandao.

“Ninataka kumwambia kila mmoja kuwa nitawahudumia watu wote bila kujali ikiwa walinipigia kura au la. Nitawapigania pamoja na familia zenu,” akasema.

Warnock atashiriki tena katika uchaguzi mwaka ujao, kwani uchaguzi huo ulikuwa wa kujaza miaka miwili iliyobaki.

Kwenye uchaguzi wa kwanza uliofanyika jimboni humo mnamo 2016, Johnny Isackson wa Republican ndiye aliyeibuka mshindi. Hata hivyo, alijiondoa kama seneta mwaka 2020 na nafasi hiyo kushikiliwa kwa muda na Loeffler.

Matokeo hayo ni pigo kubwa kwa Rais Trump, kwani Republican ndiyo imekuwa ikidhibiti siasa za jimbo hilo kwa muda mrefu. Kwenye uchaguzi wa Novemba, Biden alimshinda Trump kwa kura 11,779 hali iliyomfanya Biden kuwa mwaniaji wa kwanza wa Democratic kupata ushindi wa hapo tangu mwaka 1992.

Wadadisi wa siasa nchini humo wanasema matokeo hayo yanaonyesha jinsi Democratic inavyoendelea kupata umaarufu kwa kasi.

Hata kabla ya uchaguzi huo kufanywa, watu milioni tatu walikuwa washapiga kura kwa njia ya barua.

Idadi hiyo ilijumuisha ongezeko la wapigakura wapya 120,000 ambao hawakushiriki kwenye uchaguzi huo Novemba.

Kijumla, kulikuwa na ongezeko la wapigakura milioni moja.

Idadi hiyo inatajwa kuwa ya kihistoria kwani kwa kawaida, si watu wengi hujitokeza kushiriki kwenye duru za pili za uchaguzi.

  • Tags

You can share this post!

KING’ORI: Wapwani waunde chama kutetea maslahi yao...

Shirika lataka IEBC izuiwe kukagua saini