• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Covid: China yatoa vyeti vya chanjo kwa wasafiri

Covid: China yatoa vyeti vya chanjo kwa wasafiri

Na MASHIRIKA

BEIJING, China

CHINA imezindua mpango wa kutoa vyeti vya afya kwa raia wake na kuwa taifa la kwanza duniani kuanzisha utoaji wa vyeti vinavyofahamika kama pasipoti za virusi.

Katika siku za usoni, baadhi ya mataifa huenda yakahitaji ushahidi wa kupokea chanjo ili kuruhusu watu kuingia.

Raia watapata cheti hicho cha kidijitali, kinachoonyesha iwapo mtu amepokea chanjo au la na matokeo ya vipimo vya virusi hivyo, kupitia tovuti kwenye mtandao wa kijamii Uchina, inayofahamika kama WeChat, iliyoanzishwa Jumatatu.

“Cheti hiki kimezinduliwa ili kusaidia kuboresha ufufuzi wa mifumo ya kiuchumi ulimwenguni na kuwezesha usafiri baina ya mataifa,” msemaji wa wizara ya masuala ya kigeni alisema.

Hata hivyo, cheti hicho cha kimataifa cha afya kwa sasa kinapatikana tu kwa matumizi ya raia wa Uchina na bado hakijakuwa cha lazima.

Cheti hicho ambacho vilevile kinapatikana kama nakala, kimetajwa kama ‘pasipoti ya kwanza ya virusi’ inayofahamika duniani.

Amerika na Uingereza ni miongoni mwa nchi ambazo kwa sasa zinatafakari kuanzisha idhini kama hizo.

Umoja wa Uropa pia unajitahidi kuanzisha “kibali” cha virusi kitakachoruhusu raia kusafiri katika mataifa ambayo ni wanachama na kwingineko.

Mfumo wa Uchina unajumuisha nambari inayoweza kusomwa kielektroniki inayoruhusu kila taifa kupata taarifa ya afya ya mtumiaji, ripoti nchini humo zilieleza Jumatatu.

Tayari “nambari za kielektroniki” katika WeChat na programu nyinginezo za simu zinahitajika ili kuruhusiwa kuingia na kusafiri katika maeneo mengi ya umma nchini humo.

Appu hizo hufuatilia eneo ambapo mtumiaji yupo na kutoa nambari ya “kijani kibichi” ambayo ni sawa na kusema mtumiaji ana afya njema, ikiwa hajakuwa karibu na kisa kilichothibitishwa au hajasafiri katika eneo lenye visa vingi vya virusi.

Mfumo huo umeibua wasiwasi kuhusu usalama wa habari za siri huku kukiwa na hofu kwamba utazidisha kufuatiliwa na serikali.

Si kila mtu amefurahishwa na wazo la pasipoti za chanjo.

Mswada unaotaka serikali ya Uingereza kutoanzisha vyeti hivyo umetiwa sahihi na watu zaidi ya 200,000, kumaanisha kuwa utawasilishwa kujadiliwa na wabunge.

“Ikiwa taifa lingine litasema usiingie kama haujapokea chanjo, basi tunataka raia wa Uingereza kuonyesha hivyo,” alisema Katibu wa Wizara ya Afya Matt Hancock.

Nchi ya Cyprus imesema kuwa raia wa Uingereza ambao wamepokea dozi mbili za chanjo wanaweza kuingia nchini humo kuanzia Mei 1.

You can share this post!

Wababaisha ‘Baba’

Jombi ‘afilisisha’ shugamami