• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
DRC yatangaza kuzuka kwa maradhi ya Ebola

DRC yatangaza kuzuka kwa maradhi ya Ebola

NA MASHIRIKA

KINSHASA, DRC

MAAFISA wa serikali nchini DR Congo wametangaza kuzuka kwa maradhi hatari ya Ebola, baada ya kisa kimoja kugunduliwa katika mji wa Mbandaka, mkoani Equateur.

Huo ndio mkurupuko wa tatu wa maradhi hayo katika mkoa huo tangu 2018.

Idara ya afya nchini humo ilisema kuwa kufikia sasa ni kisa kimoja pekee cha maradhi hayo ambacho kimethibitishwa.

Mwathiriwa, ambaye ni mwanamume wa umri wa miaka 31, alianza kuhisi dalili mnamo Aprili 5, baada ya kukaa nyumbani kwa wiki moja akipokea matibabu.

Baadaye, aliamua kutafuta matibabu katika kituo cha afya kilicho karibu.

Alhamisi iliyopita, alilazwa katika kituo maalum cha kukabili maradhi ya ebola, lakini akafariki.

Baada ya kubaini dalili alizokuwa nazo, wahudumu wa afya walichukua sampuli kadhaa kutoka kwake ili kufanyiwa utafiti.

Maafisa hao walisema serikali inaendelea na uchunguzi kubaini asili ya kisa hicho na kiwango cha maambukizi nchini humo.

“Hatuna muda wa kutosha,” akasema Dkt Matshidiso Moeti, ambaye ndiye mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) barani Afrika.

“Maradhi hayo yamedumu kwa muda wa wiki mbili katika eneo hili. Tunajaribu tuwezavyo kuona ikiwa tutadhibiti athari zake. Cha kuridhisha ni kuwa, taasisi na wahudumu wa afya nchini DRC wana uzoefu wa kukabili visa vya maradhi hayo,” akaeleza.

Mkurupuko huo ni wa 14 kuibuka nchini humo tangu 1976 na wa sita tangu 2018.

Maradhi hayo ualilipuka katika mkoa wa Equator miaka ya 2020 na 2018, ambapo visa 130 na 54 vilithibitishwa mtawalia.WHO ilisema kuwa juhudi za kubaini kiwango cha maambukizi ya virusi hivyo zinaendelea.

Ripoti zilieleza kuwa mwathiriwa alizikwa kwenye mazishi yaliyozingatia taratibu maalum ili kupunguza uwezekano wowote wa maambukizi hayo kuongezeka.

Vile vile, idara za afya zinawatafuta watu waliotangamana na mwathiriwa ili kutenganishwa na raia wengine.Kituo ambako mwathiriwa huyo alilazwa pia kimenyunyiziwa dawa za kuua virusi.

Wataalamu wa WHO nchini humo wanazisaidia taasisi za afya kuendesha mikakati ya kubaini na kudhibiti maambukizi ya virusi vya maradhi hayo.

Shughuli hizo zinashirikisha kuwakagua watu ikiwa wameambukizwa, kuwatafuta wale waliotanganana na waathiriwa, kuwatibu na kushirikiana na jamii ili kuvisaidia vituo vya afya kuendesha juhudi za kudhibiti maambukizi.

Utoaji chanjo dhidi ya maradhi hayo umepangwa kuanza rasmi katika siku kadha zijazo.Serikali ilisema taifa hilo tayari lina akiba ya kutosha ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo, aina ya rVSV-ZEBOV, hasa katika miji ya Goma na Kinshasa.

Chanjo hizo zimepangiwa kusafirishwa katika eneo la Mbandaka ili wenyeji kuanza kuchanjwa mara moja.

“Tayari, watu wengi katika eneo hilo wamepewa chanjo hizo. Hivyo, tunatarajia juhudi zetu zitatuwezesha kukabili makali ya maradhi hayo,” akasema Dkt Moeti.

Akaongeza: “Wale ambao walichanjwa wakati wa mchipuko wa ugonjwa huo 2020 watachanjwa tena.”

Ebola ni maradhi hatari ambayo huwaathiri binadamu na wanyama.

Athari zake huwa hatari, hasa ikiwa mwathiriwa huwa hapati matibabu ya haraka.

  • Tags

You can share this post!

Macron ashinda duru ya pili ya uchaguzi wa urais

Pigo kwa Asha, Zamzam akitwaa tikiti ya ODM

T L