• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Hofu vita vya Ukraine, Urusi kuchukua miaka

Hofu vita vya Ukraine, Urusi kuchukua miaka

NA MASHIRIKA

BERLIN, UJERUMANI

HUENDA vita vinavyoendelea kati ya Ukraine na Urusi vikadumu kwa miaka kadhaa, limeonya Shirika la Kujihami (NATO).

Kulingana na Katibu Mkuu wa shirika hilo, Jens Stoltenberg, ni lazima mataifa ya Ulaya yawe tayari kuendelea kuisaidia Ukraine.

Katibu huyo alisema kuwa gharama ya vita hivyo ni ya juu, “na lazima dunia iwe tayari kukabili athari zake.”

Kauli yake ilijiri muda mfupi baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, kutoa matamshi kama hayo.

Wawili hao walisema kuwa Ukraine itaibuka mshindi dhidi ya Urusi tu, ikiwa mataifa mengi yatajitolea kutuma silaha zaidi kuisaidia.

“Lazima tujitayarishe kuwa huenda vita hivi vikachukua miaka kadhaa ili kukamilika. Tunapaswa kuendelea kuisaidia na kuiunga mkono Ukraine,” akasema Stoltenberg, kwenye mahojiano na gazeti la Bild, nchini Ujerumani.

“Gharama ya vita hivi inaongezeka kutokana na kupanda kwa bei ya chakula na mafuta,” akaongeza.

Mkuu huyo alisema kuwa ikiwa mataifa ya Magharibi yataitikia wito wa kuisaidia Ukraine kwa silaha za kisasa, hilo litaongeza uwezo wake wa kukomboa eneo la Donbas, ambalo himaya yake kubwa iko chini ya udhibiti wa Urusi.

MAKABILIANO MAKALI

Kwa miezi michache iliyopita, vikosi vya Urusi na Ukraine vimekuwa vikikabiliana vikali kwenye juhudi za kuchukua udhibiti wa eneo hilo.

Hata hivyo, ripoti zilieleza kuwa Urusi imekuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vikosi vya Ukraine.

Kwenye makala aliyoandika jana kwenye gazeti la ‘The Sunday Times’, Johnson alimkashifu vikali Rais Vladimir Putin wa Urusi kwa kutumia njia za kikatili, hata baada ya kuonekana kupata ushindi kwenye vita hivyo.

“Ninahofia huenda tunapaswa kujitayarisha vita hivi kuendelea kwa muda mrefu. Uamuzi mkuu kuhusu mwelekeo ambao vita hivi vitachukua ni ikiwa Ukraine itaimarisha uwezo wake kuitetea himaya yake na ikiwa Urusi itaimarisha mashambulio yake,” akasema Johnson.

Johnson, ambaye alizuru Ukraine mnamo Ijumaa, alisema kuwa njia za pekee ambazo zitaisaidia Ukraine kukabili uvamizi huo ni usaidizi wa silaha za kisasa na utoaji mafunzo kwa wanajeshi wake.

Katika siku za hivi karibuni, maafisa wa serikali ya Ukraine wamekuwa wakieleza kuhusu haja ya kulisaidia taifa hilo kwa silaha.

Wamekuwa wakisema kuwa hiyo ndiyo njia pekee itakayoviwezesha vikosi vyake kuyashinda majeshi ya Urusi.

Jumatano, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksiy Resnikov, alikutana na wawakilishi wa zaidi ya nchi 50 jijini Brussels, nchini Ubelgiji, ili kuomba usaidizi wa silaha zaidi.

Ijapokuwa mataifa kadhaa ya Magharibi yameahidi kutoa usaidizi wa silaha, Ukraine ilisema imepokea silaha chache tu ikilinganishwa na ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa.

Kwenye kikao hicho, ilisema inahitaji silaha za kisasa ili kuimarisha juhudi za kuikabili Urusi.

Wakati huo huo, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine jana alifanya ziara yake ya kwanza katika eneo la Kusini, ambalo limekuwa ngome ya makabiliano makali kati ya vikosi vyake na Ukraine.

Zelensky alizuru mji wa Mykolaiv, ambapo alikagua majengo yaliyoharibika. Baadaye, alikutana na majeshi, maafisa wa serikali na wahudumu wa afya.

  • Tags

You can share this post!

WANTO WARUI: Masomo ya sanaa, utendaji katika CBC bado...

TALANTA: Michoro yake ni hadithi tamu

T L