• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
ICC yatoa agizo Putin akamatwe kwa uhalifu

ICC yatoa agizo Putin akamatwe kwa uhalifu

NA MASHIRIKA

THE HAGUE, UHOLANZI

MAHAKAMA ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) imetoa agizo la kukamatwa kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kwa tuhuma za kuendeleza uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

Kwenye taarifa iliyotolewa Ijumaa, mahakama hiyo yenye makao yake makuu jijini The Hague nchini Uhalonzi, ilisema Rais Putin “anadaiwa kuwajibika kwa uhalifu wa kivita na uhamishaji wa watoto kinyume cha sheria kutoka maeneo yanayoishi watu nchini Ukraine na kuwasafirisha hadi nchini Urusi”.

Mahakama hiyo ya ICC pia ilitoa agizo la kukamatwa kwa Maria Alekseyevna Lvova-Belova, ambaye ni kamishna wa haki za watoto katika afisi ya Rais Putin kwa tuhuma sawa na hizo.

Serikali ya Urusi haikutoa kauli yoyote kufuatia hatua hiyo ya mahakama ya ICC.
Hata hivyo, Urusi imekana madai kuwa imetekeleza maovu na vitendo vya ukiukaji haki tangu ilipovamia Ukraine mnamo Februari 24, 2022.

Agizo hilo la kukamatwa kwa Putin limejiri siku moja baada ya uchunguzi ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN), kutoa ripoti iliyosema kuwa Urusi ilitekeleza aina kadha za uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

Ripoti hiyo ilitaja usafirishaji kwa nguvu wa watoto kutoka maeneo nchini Ukraine yanayodhibitiwa na wanajeshi wa Urusi na kusafirishwa hadi Moscow.

Mnamo Septemba 2022, Urusi ilidai kuwa raia wa maeneo ambayo iliteka kutoka Ukraine, walipitisha kura ya kuwa raia wa Urusi, huku Ukraine na washirika wake wakishtumu hatua hiyo kama ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Kulingana na Urusi, maeneo hayo manne ya Donetsk, Luhansk, Zaporizhia na Kherson, ambayo kwa jumla ni asilimia 15 ya Ukraine, sasa ni sehemu ya Urusi.

Maafisa wa Luhansk wanaoungwa mkono na Urusi walitangaza kuwa asilimia 98 ya wakazi walipiga kura ya kujiunga na Urusi, Zaporizhia (asilimia 93), Kherson (asilimia 87) na Donetsk asilimia 99.

Kura hiyo ya maoni ilifanyika nyumba kwa nyumba katika kile Ukraine ilitaja wakati huo kuwa shughuli iliyoendeshwa kimabavu katika njama ya Urusi ya kuteka maeneo yake.

Wadadisi walisema Rais Putin wa Urusi angetumia kisingizio kuwa mashambulizi katika maeneo hayo ni uvamizi wa ardhi yake. Baadaye Oktoba, Urusi ilianzisha mashambulio yaliyolenga vituo vya kuzalishia kawi nchini Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema mashambulio hayo yalivilenga vituo kadhaa katika maeneo ya magharibi, kati, kusini na mashariki. Zaidi ya makazi 1.5 milioni yaliachwa bila umeme.

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine tayari umechangia kupanda kwa gharama ya maisha ulimwenguni.

Bei ya mafuta imepanda hadi dola 100 kwa pipa na kufikia kiwango cha juu zaidi tangu 2014.

  • Tags

You can share this post!

Raila alegeza kasi ya maandamano kuenda Ikulu

Gachagua: Kenyatta na Raila wana nia Kenya iwe maskini

T L