• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 11:13 AM
Gachagua: Kenyatta na Raila wana nia Kenya iwe maskini

Gachagua: Kenyatta na Raila wana nia Kenya iwe maskini

NA LABAAN SHABAAN 

NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua ameendeleza mashambulizi yake kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta pamoja na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga akisema nia yao ni kuifanya Kenya kuwa maskini.

Bw Gachagua alidai Jumamosi kwamba rais mstaafu, ni miongoni mwa wafadhili wa maandamano yatakayofanyika Jumatatu, Machi 20, 2023 jijini Nairobi.

Muungano wa Azimio la Umoja – One Kenya, unaoongozwa na Raila Odinga ndio umepanga maandamano hayo ukiiwekea serikali ya Kenya Kwanza matakwa kadha wa kadha.

Akizungumza katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kianyaga, iliyoko Kaunti ya Kirinyaga aliposhiriki hafla ya wanafunzi wa zamani, Naibu Rais alikashifu Raila akidai anashirikiana na Kenyatta kufanya nchi kuwa fukara kupitia maandamano ya Jumatatu.

Gachagua aidha alitumia jukwaa la ziara yake Kianyaga kuhakikishia wafanyabiashara jijini Nairobi usalama wa mali yao, akisema mikakati maalum imewekwa kudhibiti vurugu.

“Mipango ya kutosha imewekwa kulinda maisha na mali Jumatatu, na ningependa kuambia watu waendelee na biashara zao,” alisema.

Naibu Rais Rigathi Gachagua adai nia ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga ni kufanya Kenya kuwa maskini kupitia maandamano. PICHA / MAKTABA

Chini ya usukani wa Rais William Ruto, Gachagua alisema nchi ni imara, na kwamba ‘makuhani’ wenye nia kutikisa uchumi na serikali hawatafaulu kuvunja sheria ‘wakijificha’ nyuma ya maandamano.

Bw Kenyatta amepata shinikizo akitakiwa kuelezea msimamo wake kuhusu maandamano ya Azimio.

Kauli ya Gachagua kuhusu ufadhili wa maandamano, wakati wa ziara yake Kianyaga ilikuwa imetajwa na kiongozi wa wengi wa bunge la kitaifa Kimani Ichungwa, mwenzake wa seneti Aaron Cheruiyot na mbunge wa Naivasha, Jayne Kihara.

Hayo yakijiri, Bw Raila ameonekana kulegeza kamba kuhusu tishio la kuelekea Ikulu.

“Kama Rais atakuwa Harambee House tutapeleka huko, kama atakuwa Ikulu tutatuma ujumbe wa watu wachache wampelekee rufaa yetu, si umati,” alisema.

Na endapo matakwa ya Azimio hayatatekelezwa, kiongozi huyo wa ODM alisisitiza kwamba Jumatatu haitakuwa mwisho wa maandamano.

Upinzani unashinikiza serikali kushusha gharama ya maisha mara moja, sava ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufunguliwa na uundaji wa tume mpya ya uchaguzi kusitishwa, Bw Raila akipendekeza makamishna waliojiuzulu na kutimuliwa warejeshwe.

  • Tags

You can share this post!

ICC yatoa agizo Putin akamatwe kwa uhalifu

JAMVI LA SIASA: Gachagua alia ugumu wa ‘kukomboa’ Mlima

T L