• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:11 PM
Jaji asukumia Koome kesi ya Sheria ya Fedha 2023

Jaji asukumia Koome kesi ya Sheria ya Fedha 2023

NA RICHARD MUNGUTI

MACHO ya Wakenya sasa yanamuelekea Jaji Mkuu Martha Koome, anayetarajiwa kupokea faili ya kesi kuhusu Sheria ya fedha ya mwaka 2023.

Jumatatu, Julai 10, 2023, Jaji Mugure Thande aliendeleza marufuku ya utekelezaji Sheria hiyo iliyopaswa kuanza Julai 1.

Kesi hiyo iliwasilishwa na Seneta wa Busia, Okiya Omtatah.

Akisitisha utozaji ushuru mpya na serikali, Jaji Thande alisema kesi hiyo ya Omtatah kuhusu uhalali wa sheria hii ya Fedha 2023 inahitaji kusikizwa na kuamuliwa na majaji watatu watakaoteuliwa na Jaji Mkuu Koome.

“Baada ya kusikiza ushahidi wa Omtatah na Serikali, nimeridhika walalamishi wameibua masuala nyeti kuhusu uhalali wa Sheria ya Fedha 2023. Nakubaliana nao kwamba sheria hiyo ina kasoro tele,” akasema Jaji Thande, akitoa mwelekeo kuhusu kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii.

Aliagiza kesi hiyo ipelekwe kwa Jaji Koome atakayeteua majaji watatu.

Ni hao watakaoamua kama Bunge la Kitaifa lilivunja sheria kutopelekwa Mswada wa Fedha 2023 kuidhinishwa na bunge la Seneti.

Na wakati huo huo Jaji Thande alitupilia mbali ombi la Serikali na Mabunge yote mawili yaliyomtaka asitishe agizo lake la kuzuia ukusanyaji wa kodi kwa madai huduma za serikali zitakwama.

“Siwezi sitisha agizo nililotoa Juni 30, nikipiga breki wananchi kutozwa ushuru mpya nitakuwa nafanya ubatili tu. Wananchi hawatalipa kodi hii mpya hadi majaji watatu watakapoamua uhalali wa sheria hii mpya ya ushuru,” akasema.

Sheria hiyo ilitiwa saini na Rais William Ruto Juni 26.

Akifafanulia serikali utafsiri wa agizo lake, Jaji Thande alisema inamaanisha hakuna kulipa ushuru mpya.

Ushuru wa zamani ndio utakaoendelea kutozwa wananchi.

Jaji huyo pia aliagiza kesi nyingine tisa za kupinga sheria hiyo mpya zikiwamo za muungano wa Azimio na chama cha mawakili nchini (LSK) zipelekwe kwa Jaji Koome kupewa mwelekeo.

Azimio na LSK kupitia kwa mawikili Paul Mwangi na Eric Theuri mtawalia walipinga utekelezwaji wa sheria hiyo mpya wakisema ilipitishwa na bunge la kitaifa na kupelekwa kutiwa sahihi na Rais Ruto kimakosa.

Katika kesi hizo 10, mahakama kuu imeombwa iharamishe sheria hiyo ya Fedha 2023 kwa vile inashurutisha wafanyakazi wa serikali kulipa kodi ya asilimia tatu (3%).

Mahakama ilikubaliana na madai ya Omtatah kwamba Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula alikosa kutopeleka mswada wa Fedha katika bunge la Seneti kujadiliwa na kuidhinishwa.

Jaji huyo alisema ushahidi aliowasilisha Omtatah umeonyesha mswada wa fedha unahusu serikali za kaunti na lazima ungelijadiliwa na bunge la Seneti kabla ya kupelekwa kutiwa sahihi na Rais Ruto.

Jaji huyo alisema mahakama kuu iko na uwezo kwa mujibu wa Kifungu nambari 165 kuhoji sheria yoyote inayaodaiwa inakinzana na Katiba.

Mwanasheria mkuu Justin Muturi, kupitia kwa wakili Prof Githu Muigai alidai serikali itakuwa inapoteza Sh574 milioni kila siku kutokana na agizo hilo la kusitisha sheria hii mpya ya kutoza ushuru.

Omtatah na mawakili Otiende Amolo na Daniel Maanzo walisema sheria hii mpya inaashiria wananchi walipe Sh211bilioni zaidi kinyume cha sheria.

Mahakama ilielezwa na Amollo kuwa huduma za serikali hazitakwama na kwamba serikali itaendelea kukusanya zaidi ya Sh3.4 trilioni kufadhili bajeti yake.

Jaji Koome atawateua majaji watatu kisha kutenga siku ya kusikizwa kwa kesi hiyo.

Bw Omtata na Amollo walieleza Jaji Thande kwamba Prof Githu alikuwa anapotosha akidai agizo la kusitisha sheria hii ya Fedha 2023 itavuruga huduma na shughuli za serikali.

 

  • Tags

You can share this post!

Makahaba waliopora mwanamume Sh250, 000 Makutano ya Mwea...

DCI Murang’a: Ako wapi Esther Ruguru aliyetoweka...

T L