• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
DCI Murang’a: Ako wapi Esther Ruguru aliyetoweka Kiria-ini Julai 1, 2023?

DCI Murang’a: Ako wapi Esther Ruguru aliyetoweka Kiria-ini Julai 1, 2023?

NA MWANGI MUIRURI

MNAMO Julai 1, 2023 Bi Esther Ruguru, 43, alionekana mwendo wa saa mbili usiku akifunga biashara yake ya hoteli iliyoko katika mji wa Kiria-ini, Kaunti ya Murang’a.

Tangu siku hiyo, hajawahi kuonekana tena licha ya kwamba mashahidi wanasema alishika njia kuelekea kwake kwa miguu.

“Tunamjua vyema. Mwanamke roho safi, mkarimu na mimi ni mteja wake wa kila siku katika hoteli yake. Polisi waache mchezo na watwambie Bi Ruguru ako wapi,” asema Joseph Njogu, mwenyeji.

Bw Njogu aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “hata mbunge wetu Bw Edwin Mugo anapaswa kutusaidia kumsaka Bi Ruguru”.

Bi Ruguru ambaye ni mama wa watoto watatu wa kati ya miaka 9 na 21 anaaminika alijipata mikononi mwa mwanamume fulani.

“Mamangu hakufika nyumbani. Tulipiga simu yake lakini haikushikwa. Nikafikiria ako kwa biashara yake. Lakini sasa matumaini ya kumpata mamangu imegeuka kuwa taharuki,” akasema Bi Carolyne Njoki, 21, ambaye ni mwanawe mkubwa.

Ripoti ya kupotea kwake ilipigwa katika kituo cha polisi cha Kiria-ini na imenakiliwa kama tukio nambari 07/04/07/23.

Caroline Njeri, 21, mwanawe Bi Esther Ruguru 43 aliyetoweka Kiria-ini Kaunti ya Murang’a Julai 1, 2023. Picha|MWANGI MUIRURI

Ripoti ya uchunguzi inaonyesha kwamba Bi Ruguru huenda alipatana aidha kwa hiari au kimabavu na mmoja wa marafiki wake.

“Kuna mwanamume fulani ambaye ni mfanyabiashara katika Kaunti ya Nyeri na ambaye inaonekana walikutana usiku huo anaodaiwa kupotea. Lakini cha kushangaza ni kwamba, kwa sasa mwanamume huyo ako hospitalini akiuguza majeraha anayosema yalisababishwa na ajali ya pikipiki,” ripoti hiyo yasema.

Lakini mpelelezi mkuu katika kesi hiyo anasema kwamba uchunguzi hadi sasa umezua sadfa nyingi kuhusu wawili hao katika siku hiyo alitoweka “na uchunguzi zaidi huenda ukatupa taswira kamili ya kutoweka kwa Bi Ruguru”.

Kwa mfano, simu ya Bi Ruguru inaonekana ilizimika akiwa karibu na kwenye simu ya mwanamume huyo usiku aliotoweka.

“Ripoti ya daktari kuhusu majeraha itatupatia taswira kamili kuhusu madai yake ya kuhusika katika ajali ya barabarani akitumia pikipiki ilhali kuna ushahidi kwamba alikuwa akiendesha gari lake,” akasema.

Bi Njoki aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “sisi kama watoto wake hatutaki siasa kuhusu maisha ya mamangu. Tunachohitaji ni mamangu arejee nyumbani ili tuendelee na maisha yetu”.

Hata hivyo; “Polisi wa Kiria-ini wanadai hongo ya Sh5 ,000 ili watusaidie kumpata Bi Ruguru,” akasema Bi Jane Njeri ambaye ni mfanyabiashara mwenzake.

Alisema kwamba “huo ni utundu usiofaa wa afisa wa polisi kutojali hali ya taharuki ambayo imekumba watoto wa Bi Ruguru”.

Alisema kwamba “kuna maafisa katika kituo hicho ambao wanaongea visivyo bila ushahidi wakidai kwamba Bi Ruguru kwa sasa ni maiti na ikiwa wangekabidhiwa hongo hiyo ya Sh5, 000 wangetuonyesha maiti yake”.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Patrick Mukuria alisema kwamba ashapata habari kuhusu hali hiyo tata “na nawahakikishia wadau wote kwamba tutazidisha uchunguzi na tutoe jibu mwafaka kwa familia”.

Alisema madai ya kuitishwa hongo ni mazito sana “na ikiwa habari hizo zinaweza zikawasilishwa rasmi kwa afisi yangu nawahakikishia wahusika watakiona cha mtema kuni”.

[email protected]

 

 

  • Tags

You can share this post!

Jaji asukumia Koome kesi ya Sheria ya Fedha 2023

Bei ya maji Nairobi na Mombasa kupanda

T L