• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Kabuga kushtakiwa wiki ijayo The Hague

Kabuga kushtakiwa wiki ijayo The Hague

NA AFP

PARIS, UFARANSA

MSHUKIWA Mkuu wa mauaji ya halaiki yaliyotokea 1994 nchini Rwanda, Felicien Kabuga, atafunguliwa mashtaka jijini The Hague, Uholanzi mnamo Septemba 29.

Jaji mmoja wa mahakama ya Umoja wa Mataifa (UN) alisema kuwa Kabuga atashtakiwa kwa mauaji ya Watutsi na uhalifu wa kibinadamu.

Inadaiwa kuwa mshukiwa huo ambaye ni mmoja wa watu tajiri Rwanda, alianzisha kituo cha redio ambacho kilitumiwa kuchochea mauaji ya Watutsi na kutoa ufadhili kwa makundi ya wapiganaji.

Kabuga, 80, alikamatwa nchini Ufaransa mnamo Mei 2020 na kuhamishwa hadi mahakama ya UN jijini The Hague, Uholanzi kushtakiwa kwa kuchangia mauaji ya Watutsi.

“Mahakama inaamuru kwamba, mashtaka yaanze katika tawi lake The Hague mnamo Septemba 29, 2022. Na ushahidi utaanza kutolewa mnamo Oktoba 5,” Jaji Iain Bonomy wa mahakama hiyo inayojulikana kama, Mechanism for International Criminal Tribunal (MICT).

Akiwa amevalia suti nyeusi, tai nyeusi na shati nyeupe, Kabuga alisikiza kwa makini agizo hilo la Jaji Bonomy.

Awali, mshukiwa huyo aliingizwa mahakamani akiwa kwenye kiti cha magurudumu.

Awali, Kabuga alikuwa amepangiwa kufikishwa katika mahakama ya Arusha, Tanzania, ambako tawi jingine la MICT linapatikana. Lakini majaji wakaamua kuwa atasalia The Hague “hadi uamuzi mwingine utakapotolewa.”

Mnamo Juni 2022, majaji walitupilia ombi la mawakili wa Kabuga waliodai afya ya mteja wao imedhoofika na hafai kushtakiwa.

Mnamo Alhamisi, Jaji Bonomy alisema mshukiwa atafikishwa mahamani mara tatu kwa wiki ambapo kesi itasikizwa kwa saa mbili kila moja ya siku hizo.

Ataruhusiwa kuhudhuria vikao vya mahakama hiyo kupitia video, ikihitajika, jaji huyo alisema.

Alipoulizwa kuhutubia mahakama, Kabuga alimwambia Jaji Bonomy kwamba ,alitaka kubadilisha mawakili wake.

Kabuga alipowasilishwa kortini kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 2020, wakili wake wa sasa Emmanuel Altit alisema mteja wake hakuwa na hatia.

Kabuga anakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo moja la mauaji ya halaiki na matatu yanayohusiana na uhalifu dhidi ya binadamu.

Kabuga, ambaye alikuwa mshirika wa chama tawala nchini Rwanda 1994, alidaiwa kufadhili kubuniwa kwa kundi la wapiganaji kwa jina, “Interahanwe Hutu militia group” na kituo cha redio kwa jina Radio-Television Libre des Mille Collines (RTLM), iliyotumiwa kuchochea watu kutekeleza mauaji.

Kituo hicho cha redio pia kilifichua sehemu ambako Watutsi walijificha ambako waliandamwa na kuuawa.

  • Tags

You can share this post!

Wazazi wataka Wizara ya Elimu iongeze muda wa masomo katika...

DOUGLAS MUTUA: Ruto apalilie utangamano wa kitaifa akiingia...

T L