• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
DOUGLAS MUTUA: Ruto apalilie utangamano wa kitaifa akiingia afisini

DOUGLAS MUTUA: Ruto apalilie utangamano wa kitaifa akiingia afisini

NA DOUGLAS MUTUA

MOJAWAPO ya makala zilizozua ubishi zaidi magazetini Rais wa pili wa Kenya, marehemu Daniel Moi, alipokaribia kustaafu, iliwapiga vijembe washirika wake.

Ubishi ulizuka kwa kuwa mwandishi aliwaita watu hao mayatima wa Bw Moi, akazama zaidi kwa kueleza jinsi ambavyo maisha yao yangalikuwa baada ya 2002.

Aliyekuwa mkurugenzi wa Huduma ya Habari za Rais (PPS) Bw Lee Njiru alikuja juu na kuwatetea watu huku akieleza kuwa ni watumishi wa umma wasiofaa kubezwa.

Sawa na kila jambo linalozua mjadala miongoni mwa umma, hilo la kiongozi wa nchi kustaafu na kuwaacha mayatima wa kisiasa linatolewa maoni mbalimbali.

Wapo wanaowachukulia watu hao kama kupe wanaomfyonza ng’ombe damu hadi akachinjwa na ngozi kutandaziwa jua ili ikauke wasitanabahi mwenye damu keshachinjwa.

Walio na mtazamo huu mara nyingi huwa ni, ama maadui wa kisiasa wa watu hao, au mahasidi tu wasio na sababu, yaani wapenzi wa kuchukia na kubeza tu kwa raha zao.

Wapo pia wanaowachukuliwa mayatima wa kisiasa kama wataalamu waliobobea kwenye masuala ya utawala, wengi wa tajiriba muhimu kwa nchi.

Lisilopingika ni kwamba, mayatima wa kiongozi wa nchi anayeondoka hukumbwa na hali ngeni, hasa ikiwa wamekuwa serikalini kwa muda mrefu.

Hawajui iwapo mustakabali wa maisha yao una hakika, iwapo zile nafasi za kutamba na kujishasha, kisa na maana mamlaka, zitarejea tena.

Kuu zaidi ni kwamba, mayatima hao huwa na hofu, wakijikuna vichwa na kujiuliza iwapo mrithi wa aliyekuwa mkubwa wao atawalenga na kuwanyanyasa.

Mara nyingi hofu hiyo hutokana na ufahamu wa watu hao kuwa, wakati mmoja au mwingine waliwahi kutumiwa vibaya na mkuu wao kumnyanyasa huyu ambaye sasa ndiye kiongozi mpya wa nchi.

Ama kweli hiyo ni hali ambayo hakuna mtu ambaye angetaka kukumbana nayo maishani, lakini haiepukiki kwa kuwa viongozi wamepishana tangu jadi. Hakuna anayeishi milele.

Kipindi cha mpito huwa rahisi kwa mayatima wa kisiasa ikiwa kiongozi anayeondoka na mrithi wake ni marafiki, hivyo hawabadilishani mamlaka chini ya wingu la uhasama.

Rais wa tatu wa Kenya, marehemu Mwai Kibaki, alipokea hatamu za uongozi kutoka kwa Bw Moi, ambaye alikuwa ameunyanyasa upinzani kwa muda mrefu.

Hata hivyo, upole wa Kibaki ulichangia utulivu na ukosefu wa dhuluma za wazi dhidi ya mayatima wa Moi kwa kiasi kikubwa wakati wa kipindi cha mpito.

Kibaki na Rais Kenyatta hawakuhasimiana, hivyo Bw Kenyatta alijichagulia tu watumishi wa Kibaki waliokuwa wazuri, masazo akayaachia Mungu ayajali.

Dkt Ruto, kwa kuwa ameyapitia magumu, anafaa kuwatendea Wakenya wote, hata Rais Kenyatta, jinsi ambavyo mwenyewe angependa kutendewa akistaafu.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kabuga kushtakiwa wiki ijayo The Hague

WANDERI KAMAU: Uhuru aige watangulizi wake kwa kumkabidhi...

T L