• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Kambi yafungwa ili kudhibiti corona

Kambi yafungwa ili kudhibiti corona

JAMES MURIMI na MASHIRIKA

WAFANYAKAZI 550 kutoka Kenya wanaohudumu katika Kituo cha Mafunzo cha Wanajeshi wa Uingereza (BATUK), kilicho Nanyuki, watalazimika kufanyia kazi kutoka majumbani mwao, baada ya wanajeshi kadhaa kuthibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Wanajeshi hao ni wale walikuwa wakihudumu katika kambi ya Nyati, iliyo katika kituo hicho, Kaunti ya Laikipia.

Ubalozi wa Uingereza nchini ulithibitisha habari hizo na kusema tayari, wanajeshi kadhaa wamewekwa kwenye karantini.

Wanajeshi hao walirejea nchini wiki iliyopita ili kuendelea na mafunzo yao, baada ya kuagizwa kurudi Uingereza mnamo Machi kufuatia kuchipuka kwa janga hilo.

Ongezeko la maambukizi ya virusi liliilazimu Uingereza kuwahamisha wanajeshi wake wote na familia zao kutoka Nanyuki ili kuwalinda dhidi ya kuambukizwa.

“Kutokana na juhudi kali ambazo tumekuwa tukiendesha dhidi ya janga hilo, tumethibitisha visa kadhaa miongoni mwa wanajeshi wanaohudumu katika kituo cha Batuk. Baadhi yao wako kwenye karantini na wataruhusiwa kutoka baada ya kuthibitishwa kupona. Tunashirikiana na idara husika na jamii katika eneo hilo ili kudhibiti maambukizi,” akasema Jumatatu balozi wa Uingereza nchini, Jane Marriot kwenye mtandao wa Twitter.

Mkuu wa mawasiliano katika ubalozi huo, Bi Janet Sudi, alisema wanajeshi wote wanaowasili nchini kutoka Uingereza ni lazima wapimwe ikiwa wameambukizwa. Vile vile, lazima wawekwe kwenye karantini kwa muda wa siku sita, kulingana na taratibu ambazo zimetolewa na serikali za Uingereza na Kenya.

Wakiwa kwenye karantini, wanajeshi hao wanakaguliwa mara kwa mara kuhusu hali yao ya afya kabla ya kuruhusiwa kuondoka.

“Juhudi na ushirikiano wa pamoja tunaoendeleza na serikali ya kaunti, idara za afya na Jeshi la Kenya (KDF) zimetusaidia sana kudhibiti athari za maambukizi,” akasema Bi Sudi, kwa niaba ya ubalozi huo.

Wiki iliyopita, hofu ilitanda Uingereza baada ya virusi ‘vipya’ vya corona, vinavyotajwa kuwa hatari zaidi kubainika katika baadhi ya sehemu nchini humo.

Tafiti kadhaa zimeonyesha kuwa virusi hivyo, vinavyoitwa E484K, vinafanana na vingine ambavyo vimebainika nchini Afrika Kusini.

Wanasayansi wamekuwa wakijaribu kubaini kuhusu ikiwa virusi hivyo vinaweza kukabiliwa kwa chanjo mpya zinazoendelea kutolewa katika nchi mbalimbali duniani. Chanjo hizo zinatumiwa kukabili muundo wa awali wa virusi hivyo.

Hapo jana, Afrika Kusini ilisimamisha kwa muda utoaji chanjo aina ya AstraZeneca, baada ya hofu kuibuka kwamba haina uwezo wa kukabili aina mpya ya virusi.

Tafiti zilionyesha chanjo hiyo inamlinda mtu “kwa kiwango kidogo tu” dhidi ya virusi hivyo vipya.

Hali hiyo imetajwa kuwa kikwazo kwenye juhudi zinazoendeshwa na taasisi mbalimbali duniani kukabili kusambaa kwa virusi.

Hilo pia ni pigo kubwa kwa mataifa maskini ambayo yalikuwa yakitegemea chanjo aina ya AstraZeneca kuwapa raia wake.

Waziri wa Afya nchini humo, Zweli Mkhize, alisema watasimamisha utoaji chanjo hiyo hadi pale watapata maelezo ya kutosha kutoka kwa wataalamu kuhusu matatizo ambayo yameibuka kuihusu.

You can share this post!

Mume, 55, achapa mamaye akitaka kujua babaye

Mafuriko yaua 18, wengine 200 hawajulikani walipo