• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Mafuriko yaua 18, wengine 200 hawajulikani walipo

Mafuriko yaua 18, wengine 200 hawajulikani walipo

Na AFP

RISHIKESH, India

WATU 18 wamethibitishwa kufariki na wengine 200 hawajulikani waliko baada ya kusombwa na mafuriko yaliyotokea baada ya jiwe la barafu kuporomoka kutoka katika safu ya milima ya Himalaya.

Jiwe hilo la barafu liliporomoka Jumapili asubuhi na kuharibu madaraja, barabara na mabwawa mawili ya kuzalishia umeme.

“Kulikuwa na kishindo kikubwa sawa na tetemeko la ardhi wakati wa kuporomoka kwa jiwe hilo la barafu,” mkazi wa eneo la Omo Agarwal alinukuliwa akisema.

Serikali ya jimbo la Uttarakhand ilisema Jumatatu kuwa miili ya watu 18 tayari imepatikana na waziri mkuu wa jimbo hilo, Trivendra Singh Rawat alithibitisha kuwa zaidi ya watu 200 hawajulikani waliko.

Wengi wa waliotoweka ni wafanyakazi wa vituo viwili vya kuzalisha umeme. Inasadikiwa kuwa baadhi ya waathiriwa wangali wamefunikwa kwa matope na mawe yaliyokuwa yakibingirishwa na mafuriko hayo.

“Maafa yaliyosababishwa na mafuriko hayo yangepungua kwa kiasi kikubwa iwapo maporomoko hayo yangetokea jioni baada ya watu kutoka kazini,” akasema Rawat.

Watu 12 waliokolewa kutoka kwenye moja ya mitaro Jumapili. Lakini watu wengine kati ya 25 na 35 walikuwa wangali wamekwama katika mtaro wa pili, kulingana na mkuu wa masuala wa mikasa wa jimbo hilo, Piyoosh Rautela.

Shughuli ya kuokoa waathiriwa ilipata pigo kutokana na barabara kuharibiwa na tukio hilo, huku wanajeshi wakilazimika kutumia kamba kupanda juu ya mlima kufikia lango za vituo vya kuzalisha umeme.

Wanajeshi na maafisa wa mikasa ya dharura kufikia jana walikuwa wakitumia trekta na vifaa vinginevyo kuondoa tope, miamba na takataka ili kufikia vituo hivyo vya kuzalishia umeme.

Kulingana na maafisa wa uokoaji, kelele za waathiriwa zimekuwa zikisikika; kumaanisha kuwa kuna watu wengi ambao wangali hai.

Serikali ilisema kuwa mafuriko hayo yalitokea baada ya jiwe hilo la barafu kuanguka ndani ya mto.

Barafu nchini India imekuwa ikiyeyuka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni kutokana na ongezeko la joto duniani. Lakini wataalamu wanasema kuwa ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme katika eneo hilo pia huenda kulichangia mawe ya barafu kuwa dhaifu na kuishia kuporomoka.

Mkasa sawa na huo ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 6,000 mnamo 2013 – hali iliyosababisha wataalamu kutaka mradi huo wa mabwawa ya kuzalisha umeme ulio katika jimbo la Uttarakhand lililoko katika mpaka wa Tibet na Nepal, ufutiliwe mbali.

Matokeo ya utafiti uliofanywa 2019 yalionyesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya barafu katika safu ya milima ya Himalaya itayeyuka kufikia 2100.

You can share this post!

Kambi yafungwa ili kudhibiti corona

TAHARIRI: Vikao vya bunge viwafae Wakenya