• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Kilio ulimwenguni bei ya mafuta ikizidi kupanda

Kilio ulimwenguni bei ya mafuta ikizidi kupanda

NA MASHIRIKA

MAMILIONI wanaendelea kuteseka kutokana na gharama ya juu ya maisha huku bei ya mafuta ikizidi kuongezeka kote duniani.

Hali ngumu ya maisha imeweka pabaya serikali mbalimbali raia nao wakiandamana.

Nchini Tanzania, raia walipigwa na butwaa jana baada ya Mamlaka ya Kuthibiti Kawi na Huduma za Maji (Ewura), kuongeza bei ya mafuta.

Ewura iliongeza bei siku chache baada ya serikali kukopa Sh4.2 bilioni kutoka kwa Benki Kuu na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa lengo la kupunguza bei ya mafuta.

Lita moja ya petroli inauzwa kwa kati ya Ksh162.93 (Dar es Salaam) na Ksh173 (maeneo ya Kagera) kuanzia jana.

Awali, lita moja ya petroli iliuzwa kati ya Ksh151(Dar es Salaam) na Ksh167 (Kagera).

Serikali ilijitetea kuwa bei ya mafuta ingekuwa kubwa zaidi iwapo isingeingilia kati na kuchukua mkopo kutoka kwa Benki ya Dunia na IMF.

Nchini Msumbiji, maelfu ya raia waliandamana mijini kupinga gharama ya juu ya mafuta.

Maandamano hayo yalitokea siku moja baada ya serikali kuongeza bei ya mafuta.

Bei ya lita moja ya mafuta ilipanda hadi Sh158 kutoka Sh149.

Maandamano hayo yalivuruga shughuli mjini Maputo kwa saa kadhaa baada ya waandamanaji kufunga barabara kuu.

SHUGHULI ZATATIZIKA

Shughuli zilitatizika katika miji mingi ya nchini Uingereza baada ya maelfu ya watu kuandamana kupinga bei ya juu ya mafuta.

Lita moja ya petroli inauzwa kwa Sh274 nchini Uingereza kuanzia Jumapili, bei ambayo imeghadhabisha raia.

Watu 13 walikamatwa kwa kufunga barabara wakitumia magari yao katika eneo la Wales. Kulingana na polisi wa Uingereza, watu hao walikuwa wakiendesha magari yao kwa mwendo wa kasi ya chini kuliko kiwango kilichowekwa na serikali kwa lengo la kuvuruga shughuli za usafiri nchini humo.

Wakati huo huo, Chama cha upinzani nchini Afrika Kusini, Economic Freedom Fighters (EFF) chake Julius Malema, kimetishia kuandaa maandamano kupinga bei ya juu ya mafuta.

Lita moja ya petroli nchini Afrika Kusini inauzwa kwa Sh168, sawa na ongezeko la asilimia 40 ikilinganishwa na mwaka jana.

Kwingineko, serikali ya Norway inakabiliwa na kibarua kigumu kumaliza mgomo wa wafanyakazi wa kampuni za kuuza mafuta.

Wafanyakazi na wamiliki wa kampuni za kuuza mafuta waligoma Jumanne wakilalamikia kukosa wateja wa bidhaa zao.

Mgomo huo tayari umesababisha kufungwa kwa viwanda vikubwa vitatu vya kuuza mafuta nchini humo.

Chama cha Mashirika ya Ndege Afrika (AFRAA) tayari kimesema kuwa mashirika ya ndege yatapata hasara ya Sh400 bilioni mwaka huu kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta.

Mashirika ya ndege nchini Kenya tayari yamepandisha nauli katika juhudi za kupunguza hasara.

Bei ya lita moja ya mafuta ya ndege imepanda hadi Sh148 kutoka Sh100 Januari, mwaka huu.

  • Tags

You can share this post!

MWANGI MURAYA: Kiko wapi Kiswahili katika manifesto za...

Kipchumba kuwania taji la London Marathon dhidi ya Bekele,...

T L