• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Kimbunga Jobo chaishiwa nguvu baada ya kuwasili Tanzania

Kimbunga Jobo chaishiwa nguvu baada ya kuwasili Tanzania

Na LEONARD ONYANGO

TANZANIA imepata afueni baada ya kimbunga Jobo kilichokuwa kinahofiwa kuwa huenda kingesababisha maafa na uharibifu wa mali ya mabilioni kuishiwa na nguvu.

Kulingana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kimbunga hicho kiliishiwa nguvu kilipokaribia jijini Dar es Salaam kutoka Bahari ya Hindi, Jumapili alfajiri.

Mamlaka ya TMA ilisema kwamba kimbunga hicho hakitasababisha madhara yoyote kwa Tanzania.

TMA, hata hivyo, ilisema kuwa, masalia ya mawingu yaliyokuwa yameambatana na kimbunga Jobo yanaweza kusababisha mvua katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani.

“Mawingu ya mvua yaliyokuwa yameambatana na kimbunga hicho yamesambaa baharini karibu na maeneo ya kusini mwa pwani ya Tanzania na Msumbiji,” ikasema taarifa ya mamlaka ya TMA.

Awali, TMA ilikuwa imetabiri kuwa kimbunga hicho kingesababisha uharibifu mkubwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Pwani, Tanga na visiwa vya Mafia na Zanzibar.

Mamlaka hiyo ilikuwa imeshauri wakazi wa mikoa ambayo ingekumbwa na kimbunga hicho kuepuka kukaa karibu na miti, majengo yasiyo imara pamoja na wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dkt Agnes Kijazi alisema kuwa kimbunga kama hicho kilikumba Tanzania mara ya mwisho mnamo mwaka 1952.

Dkt Kijazi alisema kimbunga hicho kingesababisha mafuriko makubwa nchini Tanzania.

“Ni kwa sababu upepo huo unaweza kuambatana na mvua kubwa itakayosababisha mafuriko na baadaye ukajikuta unashindwa kurudi nyumbani,” alisema Dkt Kijazi.

You can share this post!

DINI: Tunapoishi na wenzetu tuachiane alama za moyoni,...

Kibagare Slums yajiweka pazuri kuwania ubabe wa Nairobi...