• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
Kinara ajiuzulu kwa kuzidiwa na presha

Kinara ajiuzulu kwa kuzidiwa na presha

NA MASHIRIKA

COLOMBO, SRI LANKA

WAZIRI Mkuu wa Sri Lanka Mahinda Rajapaksa amejiuzulu baada ya wananchi kuandamana wakilalamikia kuzorota kwa uchumi.

Hatua hiyo inajiri baada ya serikali ya nchi hiyo kutangaza kafyu kudhibiti makabiliano kati ya wafuasi wa Rajapaksa na waandamanaji jijini Colombo, ambao wamekuwa wakipinga utawala wake.

Watu watano wamekufa katika machafuko hayo, akiwemo mbunge wa chama tawala, huku zaidi ya watu 190 wakijeruhiwa katika jiji hilo kuu.

Kumekuwa na msururu wa maandamano jijini Colombo tangu mwezi jana, wananchi wakiisuta serikali kufuatia kupanda kwa bei za bidhaa za kimsingi na kupotea kwa umeme.

Sri Lanka, ambayo ni nchi inayozingirwa na bahari, inakabiliwa na changamoto kubwa ya kiuchumi, kuwahi kushuhudiwa tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo 1948.

Bw Rajapaksa, 76, alituma barua yake ya kujiuzulu kwa kakake mdogo Rais Gotabaya Rajapaksa, akisema anaamini kuwa hatua hiyo itakomesha fujo nchini humo.

Hata hivyo, wadadisi wanasema huenda kujiuzulu kwa kiongozi huyo kukose kuridhisha wakosoaji wa serikali ya Rais Rajapaksa akiwa amesalia mamlakani.

Kumekuwa na fununu kwamba Waziri huyo Mkuu angejiuzulu baada ya ripoti kuibuka kwamba kakake alimshauri kuwa anapaswa kujiondoa.

Kabla ya kujiuzulu, Bw Rajapaksa aliwahutubia wafuasi wake Jumatatu mwendo wa asubuhi.

Saa chache baadhi ya wafuasi wake walionekana wakiwashambulia waandamanaji waliokuwa wakipinga serikali.

Habari kuhusu kujiuzulu kwa Waziri Mkuu huyo zilipokelewa kwa furaha na bashasha katika eneo la Galle Face Green lililoko karibu na bahari.

Wananchi wa eneo hilo, ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakishinikiza kujiuzulu mamlakani kwa familia ya Rajapaksa, walionekana wakisakata densi barabarani.

Familia hiyo imesalia uongozini katika mihula tofauti kwa miongo kadha.

Hata hivyo, kujiuzulu kwa Waziri Mkuu kunaonekana kama ushindi usio mkamilifu. Wanamtaka Rais Gotabaya pia ajiondoe mamlakani.

Hata hivyo, Rais huyo hajaonyesha dalili za kujiuzulu, ishara kwamba huenda maandamano yakaendelea.

Mnamo Jumatatu, shirika la habari la AFP liliripoti kwamba risasi kadha zilifyatuliwa ndani ya makazi ya Waziri Mkuu huku polisi wakipambana kuzuia waandamana kuingia humo.

Wakati wa maandamano hayo, Bw Rajapaksa na baadhi ya washirika wake wa karibu, walikuwa wamejifungia ndani ya makazi hayo.

Awali maafisa wa polisi na wanajeshi wa kukabiliana na waandamanaji waliwekwa nje ya afisi za Waziri Mkuu na Rais jijini Colombo.

Maafisa hao walirusha vitoa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama tawala baada ya wao kuvuka mstari wa polisi na kuwashambulia, kwa vijiti, waandamanaji wa kupinga serikali.

Polisi waliletwa kuwatenganisha waandamanaji na watetezi wa serikali nje ya afisi ya Rais.

Wafuasi wa Rajapaksa waliangusha hema nje ya makazi ya Waziri Mkuu katika eneo la Temple Tree na kabla ya kushambulia wapinzani wake waliokaribia eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

Ombi mradi wa kilimo ulioanzishwa na Kibaki urejeshwe Kilifi

Wafugaji maeneo kame walia serikali imewapuuza

T L