• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 6:24 PM
Wafugaji maeneo kame walia serikali imewapuuza

Wafugaji maeneo kame walia serikali imewapuuza

NA SAMMY WAWERU

WAFUGAJI kutoka maeneo kame nchini wamelalamikia kuendelea kpuuzwa na serikali mifugo yao ikihangaishwa na kiangazi na kusombwa na mafuriko kufuatia mvua kubwa inayoshuhudiwa katika baadhi ya maeneo hayo.

Huku asilia 90 ya wakazi sehemu kame ikitegemea ufugaji, wamesema wanakadiiria hasara ya mali iliyosababishwa na majanga hayo.

Kwa sasa, wanategemea chakula cha msaada kupitia wahisani na wasamaria wema hali wanayohoji imesababishia wengi msongo wa mawazo.

Hali kadhalika, wamesema mizozo ya kijamii inayoripotiwa maeneo hayo imetokana na nyakati na hali ngumu wanayopitia.

“Nimepoteza mifugo wenye thamani ya Dola 9, 800 (sawa na Sh980, 000 pesa za Kenya), kupitia ukame na mafuriko,” akasema Tumal Galdibe.

Bw Galdibe alitoa malalamishi hayo kupitia warsha ya wadauhusika sekta ya ufugaji na mazingira ulimwenguni, iliyoandaliwa kwa njia ya mtandao wa Zoom.

Katika jukwaa la warsha hiyo, Peasant and Indigenous Press Forum, mbinu za kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo kame zilijadiliwa.

Galdibe, mfugaji-biashara kaunti ya Marsabit, alidai amejiandikisha kupitia mipango ya serikali kufidia wafugaji waliopoteza mifugo ila hajawahi kufikiwa na fedha zinazosemekana kutolewa.

Hufuga mbuzi, kondoo na ngamia.

Mwezi Aprili 2022, Bw Harry Kimtai, Katibu katika Wizara ya Mifugo, aliambia Taifa Leo kwamba serikali inajikakamua kuangazia changamoto zinazofika jamii zinazoishi maeneo kame.

Afisa huyo pia alidokeza serikali kupitia Shirika la Nyama Nchini (KMC), inanunua mifugo mpango unaolenga kuokoa wanyama waliolemewa na makali ya njaa.

“Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) yanajaribu kutuletea afueni, ila serikali imezembea. Inatoa suluhu ikiwa Nairobi.

“Mapendekezo yanayotolewa maeneo ya mijini ni vigumu kufikia waathiriwa – jamii za wafugaji maeneo kame,” Galdibe akasema, akihimiza serikali kubadilisha mifumo yake ya sheria kuangazia majanga.

Kenya ni miongoni mwa nchi tatu Upembe wa Afrika, zilizolemewa na baa la njaa na ukame.

Ripoti hiyo ni kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo, FAO – UN, athari za ukame zikichochewa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Mataifa yaliyo Kusini mwa Afrika Jangwa la Sahara, athari za tabianchi zimechangia mamilioni ya watu kukumbwa na hatari ya baa la njaa.

Nguzo ya uchumi na maendeleo nchi hizo ikiwa kilimo na ufugaji, sekta hizo zimeathirika pakubwa idadi ya wakimbizi wa hali ya hewa ikiongezeka.

  • Tags

You can share this post!

Kinara ajiuzulu kwa kuzidiwa na presha

ODM yapuuza hatua ya Kingi kuitoroka akielekea kwa Ruto

T L