• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Kundi la ADF lazidi kutisha, UG yakiri

Kundi la ADF lazidi kutisha, UG yakiri

NA JULIUS BARIGABA

KAMPALA, UGANDA

UGANDA inakabiliwa na tishio kutoka kundi la kigaidi la Allied Democratic Forces (ADF), zaidi ya mwaka mmoja baada ya kuazisha operesheni dhidi ya kundi hilo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Juzi, wapiganaji wa ADF walijaribu kuvuka mpaka kuingia Uganda kutoka DRC, hatua iliyochangia asasi za usalama kukiri kuwa nchini hiyo sasa inakabiliwa na tishio kutoka pande tatu.

Hii inaonyesha kuwa wapiganaji hao wanajikusanya ndani ya Uganda na wanapanga kufanya mashambulio kwa kutumia vilipuzi.

Aidha, awali, wanachama wa kundi hilo waliwahi kushambulia vijiji na vituo vya polisi na kusababisha vifo vya raia na maafisa kadha.

Wavamizi hao pia wamewahi kuiba bunduki 16 kutoka vituo hivyo vya polisi.

Ufichuzi huo upo kwenye ripoti moja iliyotayarishwa na kundi la wataalamu wanaofuatilia hali ya usalama nchini DRC.Ripoti hiyo iliwasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) mnamo Desemba 16.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa operesheni ya pamoja ya wanajeshi wa Uganda na wenzao wa DRC “haijafaulu kufikia malengo ya kuzima kabisa au kudhoofisha ADF.”

Ripoti hiyo inaongeza kuwa manufaa ya “Operesheni Shujaa” kama operesheni katika ya Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) na lile la DRC, yamepungua baada ya wanajeshi hao kukabiliana na shida ya uchukuzi kutokana na ubovu wa barabara ndani ya mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini, nchini DRC.

Operesheni hiyo ya pamoja ilizunduliwa mnamo Novemba 30, 2021.Wataalamu wanadai kuwa licha ya uharibifu wa baadhi ya kambi zao na baadhi ya wapiganaji wao kukamatwa, uongozi wa ADF “unasalia imara na thabiti”.

Aidha, kundi hilo la kigaidi lilirejelea katika ngome yake ya zamani, ikiwemo karibu na vituo vya UPDF nchini DRC vilivyoko karibu na mpaka wake na Uganda.Mnamo Desemba 13, kundi la wapiganaji 40 wa ADF walivuka mto Semliki na kushambulia vijiji katika eneo la Bweramule, wilaya ya Ntoroko, linalopakana na DRC, kabla ya UPDF kukabiliana nao na kuua 17 kati yao na kuteka wengine 15.

Ilidaiwa kuwa wapiganaji wengine wa ADF walikufa maji katika mto huo walipokuwa wakijaribu kurejea walikotoka.

Raia watatu walithibitishwa kuuawa katika ufyatulianaji wa risasi kati ya wanajeshi na wanamgambo hao.Wakati wa shambulio hilo, waziri wa masuala ya ndani wa Uganda Jenerali David Muhoo mnamo Novemba 30, aliwasilisha ripoti bungeni inayoonyesha kuwa mashambulio 12 yalitekelezwa dhidi ya vituo vya polisi.

Shambulio lingine lilitekelezwa katika kambi moja ya kijeshi ambapo bunduki tatu ziliibiwa miezi mitatu iliyopita.

Wachanganuzi wengine wa masuala ya usalama wanasema kambi za magaidi wa ADF zinafufuliwa kwa sababu wapiganaji wa kundi hilo wanarejea Uganda baada ya kambi zao nchini DRC kuharibiwa na wanajeshi wa UPDF.

  • Tags

You can share this post!

Onyo ukame utaendelea kwa mwaka mmoja zaidi

Wasafiri kutoka China kuzimwa

T L