• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 12:11 PM
Maajabu Meya Mexico akioa mamba

Maajabu Meya Mexico akioa mamba

MERCY KOSKEI na MASHIRIKA

MEYA wa mji mdogo Kusini mwa Mexico amewaacha wanamitandao vinywa wazi baada ya kufunga ndoa na mamba (spectacled caiman (Caiman crocodilus), katika sherehe za kitamaduni ili kuleta bahati nzuri kwa watu wake.

Victor Hugo Sosa, meya wa San Pedro Huamelula, mji wa watu wa asili ya Chontal iliyo eneo la Tehuantepec Isthmus, Mexico, alimchukua mamba huyo kwa jina Alicia Adriana kama mchumba wake

Sosa alihadi ‘mpenziwe’ kuwa mwaminifu na mkweli wanapoanza safari yao ya wanandoa na kumwita “binti wa kifalme.”

“Ninakubali kuwajibika kwa sababu tunapendana. Hilo ndilo muhimu. Huwezi kuwa na ndoa bila upendo…Ninakubali kuolewa na binti wa kifalme,” Sosa alisema wakati wa ibada hiyo.

Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke wa Caiman imefanyika Mexico kwa miaka 230, ili kuadhimisha siku ambayo makundi mawili ya wenyeji walipata amani hasa kwa ndoa.

Kulingana na tamaduni zao, ugomvi ulitatuliwa wakati mfalme wa Chontal, alipofunga ndoa na binti mfalme wa kundi la wenyeji la Huave, anayewakilishwa na mamba wa kike.

Wahuave wanaishi kando ya jimbo la Oaxaca la pwani.

Kulingana na nao, harusi ya aina hii inaruhusu pande zote “kuunganishwa na ulimwengu, kuwapa fursa ya kuomba mwenye nguvu kwa ajili ya mvua, kuota kwa mbegu, amani na maelewano baina ya wakaazi”.

Kabla ya sherehe ya harusi, mamba huyo hupelekwa nyumba kwa nyumba ili wenyeji wapate fursa ya kumbeba mikononi mwao na kucheza naye.

Wakati huo anavalishwa sketi ya kijani kibichi, kanzu ya rangi ya kupambwa mikononi na kichwani.

Baadaye, anavishwa vazi la bibi harusi  na kupelekwa kwenye ukumbi jiji kwa hafla iliyobarikiwa.

Baada ya harusi, meya hucheza na bibi harusi kwa sauti za muziki wa kitamaduni.

“Tuna furaha kwa sababu tunasherehekea muungano wa tamaduni mbili. Watu wameridhika,” Sosa aliambia Shirika la Habari la AFP.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Dereva wa teksi asimulia alivyounda faida ya Sh23 Nairobi...

Msanii Mike Rùa adai atakutangulia ufalme wa Mbinguni 

T L