• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Dereva wa teksi asimulia alivyounda faida ya Sh23 Nairobi kufuatia nyongeza ya mafuta

Dereva wa teksi asimulia alivyounda faida ya Sh23 Nairobi kufuatia nyongeza ya mafuta

NA LABAAN SHABAAN

WAHUDUMU wa teksi nchini wamelalamikia kuhusu nyongeza ya mafuta ya petroli iliyotangazwa na Mamlaka ya Kawi na Kudhibiti Petroli (EPRA) mwishoni mwa juma.

Nyongeza hiyo inatokana na kupanda kwa ushuru (VAT) unaotozwa mafuta ya petroli kutoka asilimia 8 hadi 16 baada ya kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2023 uliopendekeza.

Mhudumu wa teksi aliyejitambua kama Vincent kupitia Facebook, amesema katika mojawapo ya safari yake kusafirisha mteja jijini Nairobi baada ya mfumko wa mafuta aliunda faida ya Sh23 pekee.

Huduma nyingi za teksi zinatolewa kupitia apu.

“Usimamizi wa hizi apu za teksi unapaswa kufanya kitu kwa sababu msongo wa mawazo na uchovu unatuua sisi wahudumu. Sasa hivi kila kitu kimetufinya hadi viatu na soksi,” alisema Vincent kwa masikitiko.

“Nimebeba abiria wanne kutoka Thika Road Mall (TRM) hadi Mwiki kwa Sh230 na kwa sababu walipewa kipunguzo nililipwa Sh 173. Kampuni inayosimamia huduma ikichukua asilimia 25 ya malipo hayo,” alielezea.

Vincent anayehoji kuwa bado hajajumuisha ada ya mjazo wa simu iliyowezesha mawasiliano na mteja wake, anasema kuwa gari analotumia ni la kukodisha Sh 1, 200 kwa siku.

Kutia chumvi kwenye kidonda kinachouguza, dereva huyo analalamikia kupungua kwa wateja.

Kulingana na EPRA, kuanzia Julai 1, 2023 lita moja ya petroli itakuwa ikiuzwa Sh195.50 Nairobi, kutoka Sh. 182.04, nayo dizeli imegonga Sh179.67 juu kutoka Sh167.28.

Nayo mafuta taa yanauzwa Sh173.44 kutoka Sh161.48, kwa lita.

Nyongeza hiyo inaendelezwa licha ya mahakama kusimamisha kwa muda utekelezaji wa sheria ya fedha ya mwaka wa 2023 (ndiyo Mswada wa Fedha 2023).

Mswada huo ulipitishwa na bunge na Rais William Ruto akautia saini kuwa sheria.

 

  • Tags

You can share this post!

Mbunge apendekeza wanaoiba mali ya umma wanyongwe

Maajabu Meya Mexico akioa mamba

T L