• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Maandamano yachacha Nigeria kupinga matokeo

Maandamano yachacha Nigeria kupinga matokeo

ABUJA, NIGERIA

MAELFU ya wafuasi wa upinzani nchini Nigeria wanaandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais.

Maelfu hao wanaomuunga mkono Atiku Abubakar wa chama cha People’s Democratic Party aliyekuwa akiwania kiti hicho waliandamana hadi katika makao makuu ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wakiwa na mabango ya kupinga matokeo hayo.

Haya yanajiri siku chache baada ya Tume hiyo kumtangaza mgombea wa chama tawala cha All Progressives Congress Bola Tinubu kuwa mshindi wa kiti cha urais.

Vyama vya upinzani vinasema uchaguzi huo ulitawaliwa na wizi wa kura. Maandamano hayo yaliyoongozwa na mgombea urais Abubakar na maafisa wengine wa chama yaliandaliwa kupinga tangazo lililotolewa wiki jana na mwenyekiti wa tume hiyo Mahmood Yakubu.

Waandamanaji hao walidai kuwa Abubakar alishinda uchaguzi huo kinyume na ilivyotangazwa na tume ya INEC.

“Tuna ushahidi kwamba tulishinda uchaguzi huu. Tunaamini kuwa Yakubu hakuzingatia masuala yaliyokumba uchaguzi huu. Yeye alitangaza tu mshindi bila kuzingatia masuala kama hayo,” akasema Kola Ologbondiyan Msemaji wa kamati ya Kampeni ya urais ya PDP.

Paul Ibe, mshauri wa Abubakar kuhusu vyombo vya habari, alisema, “Huu ni uchaguzi mbaya zaidi katika historia yetu ya kidemokrasia. Kulikuwa na matarajio mengi. Wananchi wa Nigeria walikuwa wanatafuta kiongozi ambaye atawaleta pamoja na kuanza mchakato wa kuufufua uchumi wetu. Ni dhahiri kuwa uchaguzi huu ulitawaliwa na wizi.”

Hata hivyo, waandamanaji hao walizuiliwa na maafisa wa polisi waliojihami.

Kadhalika, maafisa wa tume ya INEC walikataa kuzungumza na waandamanaji hao. Kwa mujibu wa matangazo hayo, Tinubu alipata kura 8.8 milioni (asilimia 36) huku mpinzani wake mkuu Abubakar akipata asilimia 29 naye Peter Obi wa chama cha Labour akipata asilimia 25.

Kabla ya matokeo kutangazwa, Abubakar, aliirai tume hiyo kuweka matokeo kwenye tovuti yake mara moja baada ya kuyapokea. Aliwalaumu baadhi ya magavana wa majimbo kwa kujaribu kubadilisha matokeo hayo.

“Itakuwa vibaya ikiwa yeyote atajaribu kubadilisha uamuzi wa raia kwa kubadilisha matokeo ya uchaguzi,” alisema kwenye taarifa.

Uchaguzi huo uliofanyika Februari 25 umekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vurugu.

Tume hiyo ilichelewa kutangaza matokeo kinyume na ilivyoahidi kabla ya uchaguzi. Tinubu ni mmoja wa wanasiasa tajiri zaidi Nigeria, na aliahidi kufufua uchumi wa nchi hiyo ambao umezorota.

Tinubu alizoa kura kadhaa katika baadhi ya majimbo, jambo lililomuweka mstari wa mbele. Uchaguzi huo ulikumbwa na ucheleweshaji na madai ya majaribio ya wizi wa kura.

Rais huyo mpya anatarajiwa kupambana na masuala ya kuzorota kwa uchumi, ukosefu wa usalama na uboreshaji wa sekta ya afya na elimu.

  • Tags

You can share this post!

UDA hatarini ‘kujikwaa’ kama Jubilee

Serikali ilitumia 55 bilioni bila idhini

T L