• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:55 AM
Mabaki ya ndege yaopolewa ziwani

Mabaki ya ndege yaopolewa ziwani

NA AFP

BUKOBA, Tanzania

SERIKALI ya Tanzania Jumanne ilitangaza kuwa mabaki ya ndege iliyoanguka katika Ziwa Victoria yameopolewa kutoka ziwani baada ya ajali ya Jumapili.

Watu 19 walikufa katika ajali hiyo iliyohusisha ndege ya Shirika la Precision mnamo Jumapili asubuhi ilipokuwa ikikaribia kutua katika uwanja wa ndege mjini Bukoba.

Baada ya kutokea kwa ajali hiyo, wafanyakazi wa mashirika ya kushughulikia majanga, wavuvi na wakazi waliungana kuondoa manusura kutoka kwa ndege hiyo iliyozama majini.

“Tumeopoa mabaki ya ndege hiyo kutoka majini na sasa uchunguzi wa kitaalamu kubaini chanzo cha ajali hiyo unaendelea,” Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini Tanzania (TAA), ilisema kwenye taarifa.

“Uwanja wa Ndege wa Bukoba pia umefunguliwa upya kuruhusu shughuli za uchukuzi wa angani kuendelea kama kawaida,” akaongeza.

Video iliyopeperushwa kupitia vyombo vya habari nchini humo, ilionyesha mabaki ya ndege hiyo yakivutwa kwa kreni.

Hatimaye, mabaki hayo yaliwekwa katika eneo la nchi kavu. Shriki la Ndege la Precision Air, ambalo ni shirika kubwa ya ndege la kibinafsi nchini Uganda, lilisema kuwa ndege ilihusika katika ajali ilikuwa aina ya ATR 42-500.

Ilikuwa imebeba jumla ya abiria 39, akiwemo mtoto mdogo, na wahudumu wanne, ajali hiyo ilipotokea.

Watu 24 waliponea kifo kati ya 43 waliokuwa ndani ya ndege ilipoanza safari katika jiji kuu la Dar es Salaam.

Miongoni mwa waliokufa walikuwa raia mmoja wa Kenya na mwingine wa Uingereza, msemaji wa serikali Gerson Msingwa aliwaambia wanahabari mjini Bukoba.

“Tunaendelea kuwasiliana na balozi za mataifa husika ili wasafirishe miili hiyo ya raia wao,” akaeleza.

Bw Msigwa alisema wachunguzi kutoka ATR walitarajiwa kuwasili nchini Tanzania Jumanne kuungana na wenzao kutoka shirika la Precision Air na TAA, waliowasili Bukoba Jumapili.

Polisi walisema ajali hiyo ilisababishwa na hali mbaya ya anga huku serikali ya Tanzania ikilaumiwa kwa kutoa mchango finyu katika shughuli za uokoaji.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, aliahidi kuwa serikali itaweka mikakati ya kuhakikisha “usalama katika sekta ya uchukuzi wa angani.”

Shirika la Precision Air, ambalo sehemu ya umiliki wake upo mikononi mwa shirika la ndege la Kenya Airways, lilianzishwa mnamo 1993.

Huendesha safari za nchini Tanzania, ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na huduma za ukodishaji na watalii.

Ajali hiyo ilijiri miaka mitano baada ya watu 11 kuangamia ndege ya shirika la Safari Company Coastal Aviation ilipoanguka eneo la kaskazini mwa Tanzania.

Mnamo 1999, watu kadha, wakiwemo watalii wa Amerika, walikufa katika ajali ya ndege kaskazini kwa Tanzania.

Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kati ya Mbuga ya Kitaifa ya Serengeti na uwanja wa ndege wa Kilimanjaro.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi ya kuoka mkate wa maboga, tangawizi na mdalasini

Wanaharakati wataka ahadi ya Paris 2015 kukabili athari...

T L