• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Wanaharakati wataka ahadi ya Paris 2015 kukabili athari hasi za mabadiliko ya tabianchi iafikiwe

Wanaharakati wataka ahadi ya Paris 2015 kukabili athari hasi za mabadiliko ya tabianchi iafikiwe

NA SAMMY WAWERU

WANAHARAKATI kuangazia tabianchi wamezitaka serikali za mataifa kuachilia fedha walizoahidi kusaidia kukabili athari.

Ahadi hiyo ilitolewa mwaka wa 2015, katika Kongamano la Kimataifa Makala ya 21 Kuhusu Tabianchi (COP21) Paris, linaloandaliwa kila mwaka na Muungano wa Kimataifa (UN).

Serikali za nchi tajiri duniani ziliahidi kupiga jeki mataifa yanayojikokota kiuchumi kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Kupitia muungano, Pan African Climate Justice Alliance (PACJA), unaojumuisha wanaharakati wa kijamii, wasomi, makundi ya wasiojiweza, wanawake, vijana na wakulima wa mashamba madogo, wanasisitiza fedha hizo zinapaswa kuelekezwa kwa wakulima na ambao wanaendelea kuumia kutokana na athari za tabianchi.

Wanaharakati hao wanasema zitawasaidia kuangazia kero ya kiangazi, janga la kame na changamoto zinazohusishwa na tabianchi.

“Hatujapona majeraha ya tandavu ya virusi vya corona, na hivi sasa janga la ukame na upungufu wa chakula ndilo hili. Usalama wa chakula Mashariki na Afrika ya Kati ni kero, mikakati ya hali ya hewa inapaswa kuwa mjadala wa kitaifa na sekta ya kilimo kupewa kipau mbele,” Alvin Munyasia, afisa kutoka PACJA ameambia Taifa Leo, kupitia mahojiano ya kipekee.

Huku Bara Afrika likikadiriwa kuchangia asilimia 4 pekee ya gesi hatari zinazochangia tabianchi, afisa huyo amesema ahadi ya 2015 inapaswa kuafikiwa.

Katika kongamano la Paris, mataifa tajiri ulimwenguni yalikuwa yameahidi kwamba yatakuwa yakitoa kima cha Sh100 bilioni kila mwaka kama mgao kuchukua hatua kuangazia tabianchi, ahadi ambayo kufikia sasa haijatekelezwa.

“Pesa hizo zitafidia wakulima hasara inayotokana na ukame, na kufanikisha mpito wa shughuli ya kilimo inayostahimili athari za tabianchi,” Bw Munyasia akaelezea.

Ombi la PACJA limejiri siku chache kabla ya Kongamano la COP27, mwaka huu, kufanyika Misri.

Muungano huo kwa ushirikiano na Kenya Platform for Climate Governance ((KPCG), umefanikiwa kuleta pamoja wanaharakati wa mazingira kutoka nchi 51 kuhamasisha umuhimu kuangazia tabianchi.

“Ni kinaya nchi za Afrika kushiriki makongamano ya tabianchi ilhali hakuna hatua inayochukuliwa,” akasema Ann Songole, kutoka Mtandao wa Mawasiliano ya Wanawake na Maendeleo (Femnet).

Wakielezea hisia zao kuhusu utepetevu wa serikali za mataifa Afrika katika kujiandaa kukabili janga la ukame na baa la njaa, wanarakati hao aidha wanaitaka Wizara ya Kilimo na ile ya Mazingira kuimarisha utendakazi.

Nchi zinazounda Upembe wa Afrika, ndizo; Kenya, Somalia na Ethiopia, zinaendelea kuhangaishwa na janga la ukame.

Nchini, ukame uliodumu kwa karibu miaka mitatu mfululizo umechangia mifugo katika maeneo kame (ASAL) kufa njaa, mimea na nyasi kukauka wenyeji wakiishia kutegemea chakula cha msaada.

  • Tags

You can share this post!

Mabaki ya ndege yaopolewa ziwani

Marubani waanza kazi baada ya mgomo wa siku 4

T L