• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Majeshi ya Urusi yateka mji mwingine Ukraine

Majeshi ya Urusi yateka mji mwingine Ukraine

NA MASHIRIKA

KYIV, UKRAINE

JESHI la Ukraine limethibitisha kuwa vikosi vya Urusi vimeuteka mji muhimu wa Lysychansk, ulio katika eneo la Luhansk.

“Baada ya mapigano makali katika mji wa Lysychansk, majeshi ya Ukraine yaliamua kujiondoa kutoka maeneo yalimokuwa yameshikilia,” akasema mkuu wa jeshi hilo kwenye taarifa Jumatatu.

Mapema Jumatatu, Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu, alisema kuwa vikosi vyake vilifanikiwa kuuteka mji huo, hivyo kuchukua udhibiti wa eneo nzima la Luhansk.

Mkuu huyo wa jeshi alisema kuwa wanajeshi wa Ukraine waliraiwa kujiondoa ili kuokoa maisha ya raia ya wake walio katika mji huo.

“Tulifanya uamuzi wa kimakusudi kujiondoa,” akasema.

Hata hivyo, taarifa zilisema wanajeshi hao walilazimika kujiondoa baada ya kuzidiwa nguvu na vikosi vya Urusi.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine aliapa kuwa vikosi vyake vitarejea jijini humo baada ya kupokea usaidizi wa silaha kutoka kwa washirika wake.

Mapema jana, kiongozi wa nchi ya Chechen, ambayo ni mshirika wa Urusi, Ramzan Kadyrov, aliweka video iliyoonyesha wapiganaji wa nchi hiyo wakiwa katikati mwa mji wa Lysychansk.

Katika eneo la magharibi, watu sita waliuawa baada ya vikosi vya Urusi kuushambulia vikali mji wa Slovyansk. Mji huo uko katika eneo la Donetsk.

Kabla ya kuanzisha mashambulio dhidi ya Ukraine, Rais Vladimir Putin wa Urusi alisema kuwa kisheria, nchi yake ndiyo inashikilia maeneo ya Luhansk na Donetsk.

Alitaja maeneo hayo kuwa huru dhidi ya udhibiti wowote wa Ukraine. Vikosi vya Urusi vilianza kuingia katika maeneo hayo tangu 2014.

Karibu wiki moja iliyopita, vikosi vya Urusi vilichukua udhibiti wa mji wa Severodonetsk, baada ya makabiliano makali na majeshi ya Ukraine. Mji huo uliharibika kabisa kutokana na mapigano hayo.

Mji wa Lysychansk uko karibu na Severodonetsk. Miji hiyo imetenganishwa na Mto Seversky Donets.

Awali, kulikuwa na matumaini kwamba vikosi vya Ukraine vingeutumia mto huo kujilinda dhidi ya mashambulio ya Urusi.

Licha ya Urusi kuchukua udhibiti wa Lysychansk, maafisa wa serikali ya Ukraine wameonekana kulinyamazia suala hilo.

Wadadisi wanasema kuwa kutekwa kwa mji huo na vikosi vya Urusi ni pigo kubwa kwa Ukraine, hasa katika eneo la mashariki.

Wakati huo huo, Uturuki imeizuilia meli moja ya mizigo kutoka Urusi iliyokuwa ikisafirisha nafaka.

Kulingana na balozi wa Ukraine nchini Uturuki, Vasyl Bodnar, meli hiyo inazuiliwa na maafisa wa idara ya forodha.

“Tunashirikiana vizuri na Uturuki. Meli hiyo inasimama katika lango kuu la bandari,” akasema.

Meli hiyo, inayoitwa Zhibek Zholy, ilikuwa ikisafiri kutoka bandari ya Berdyansk, Ukraine, hadi katika bandari ya Karasu, nchini Uturuki.

Haikubainika mara moja zilikotolewa nafaka hizo. Hata hivyo, Urusi imekuwa ikilaumiwa kwa kuiba nafaka kutoka katika maeneo ya Ukraine inayoyashikilia, madai ambayo imekuwa ikiyakanusha.

Bandari ya Berdyansk iko katika eneo la Zaporizhzhia, kusini mwa Ukraine, karibu na Bahari ya Azov.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Manifesto hazifai kupandisha joto la...

KINYANG’ANYIRO 2022: Kaunti ya Laikipia

T L