• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Majina yaliyopendekezwa kutwaa nafasi ya Kadhi Mkuu yapingwa

Majina yaliyopendekezwa kutwaa nafasi ya Kadhi Mkuu yapingwa

NA TITUS OMINDE

KIONGOZI wa vijana wa Kiislamu Eldoret amewasilisha kesi katika Mahakama Kuu kupinga majina ya watu watano waliopendekezwa kuchukua nafasi ya Kadhi mkuu.

Mlalamishi Jamal Deriwo Omari amekosoa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kwa kuwateua wagombeaji hao kujaza nafasi hiyo, akitaja mchakato uliotumika kuwaorodhesha ulikiuka sheria.

Kupitia ombi lake mahakamani, Bw Omari ana maoni kwamba mchakato wa kuwateua watano hao unakiuka sheria za Kiislamu na Katiba ya sasa, iliyoidhinishwa 2010.

Kupitia hati yake ya kiapo, mlalamishi ameambia mahakama kwamba uteuzi huo ulibagua Waislamu kutoka jamii zingine za Kiislamu kaunti zote 47.

Analalamikia uteuzi huo kuegemea eneo moja la nchi.

“Mchakato wa kuorodhesha Kadhi Mkuu haupaswi kukiuka sheria za Kiislamu na Katiba ya Kenya ambayo inaamuru kuteuliwa kwa Kadhi Mkuu,” alisema Bw Omari katika ombi lake.

Aidha Bw Omari alipinga namna tangazo la nafasi hiyo lilivyofanyika, akidai kuwa limekiuka Kanuni za Utumishi wa Umma na Sera na Taratibu za nguvukazi za mwaka 2016.

Amesisitiza kuwa uteuzi wa Kadhi Mkuu lazima uzingatie weledi unaostahili sanjari na sheria ya nchi.

Mnamo Mei 22, 2023 JSC iliwaorodhesha Sukyan Hassan Omar, Idris Nyaboga, Athman Abdulhalim Hussein, Mohamed Abdalla na Omari Hassan Kinyua ili kupigwa msasa kuhusiana na wadhifa huo.

Nafasi hiyo ilitangazwa wazi Aprili 14, 2023 na tangazo lilifungwa Aprili 28, 2023.

Tume hiyo ilisema kuna jumla ya maombi 24 yaliyowasilsihwa kabla ya kuchuja wagombea hao hadi watano.

Mahakama inatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo wiki hii.

Hii si mara ya kwanza kwa uteuzi wa Kadhi Mkuu kukabiliwa na shutuma kali.

Mwaka 2020, mwenyekiti wa kitaifa Baraza la Kitaifa la Ushauri la Waislamu wa Kenya Sheikh Juma Ngao alionya dhidi ya uajiri usio wa kawaida wa mwenye ofisi hiyo, akisisitiza kwamba Kadhi Mkuu lazima awe mtu wa hadhi ya juu katika nyanja zote lengwa.

Bw Ngao alikariri hitaji la mchujo wa haki akibainisha kuwa Waislamu kutoka kaunti zote 47 wanaohitimu wanapaswa kupewa fursa sawa akilalamika kwamba kwa muda mrefu kiti hicho kimekuwa hifadhi ya eneo la Pwani.

Wakosoaji wa uteuzi wa awali wametoa changamoto kila mara kwa JSC kushauriana na makundi yote ya Kiislamu na na wadau wote kabla kutoa mapendekezo yao.

 

  • Tags

You can share this post!

Asukumwa jela kwa kutishia kuua mamake

Taharuki magenge ya uhalifu yakihangaisha watu Nakuru

T L