• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Taharuki magenge ya uhalifu yakihangaisha watu Nakuru

Taharuki magenge ya uhalifu yakihangaisha watu Nakuru

NA MERCY KOSKEI

KAMISHINA wa Kaunti ya Nakuru Layford Kibara ametoa onyo kali kwa magenge ya uhalifu ambayo yamekuwa yakishambulia na kuwaibia wakaazi.

Bw Kibara alitoa onyo hilo baada ya visa vya utovu wa usalama kuandikisha kuongezeka kwa muda wa mwezi mmoja uliopita.

Akihutubia wanahabari Jumanne, Juni 6, 2023, afisa huyo alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la magenge haramu  katika maeneo ya Kaptebwa na Rhonda.

Kulingana na Bw Kibara, makundi yaliyoharamishwa ya Confirm, Watizedi na Mauki yamechangia uhalifu kuongezeka katika maeneo mbalimbali akisema kuwa mashambulizi yaliyoshuhudiwa majuzi yalikuwa ya kulipiza kisasi miongoni mwao.

Alisema magenge hayo ambayo yamekithiri maeneo ya Pondamali, Sewage, Top ten, Stimaline, Jasho, Grogon na Posta yametia wakazi hofu, wengi wakiogopa kuendeleza biashara zao kwa utulivu.

Kamanda wa polisi Kaunti ya Nakuru Zachary Kimani. Picha / MERCY KOSKEI

Bw Kibara alisikitika kuwa katika mashambulizi hayo, wananchi wengi wanaathirika kwani maduka yao yanavamiwa huku wengine wakiuguza majeraha.

“Tumezuru maeneo hayo na tumebaini tabia zisizo za kawaida. Wengi wanajulikana na umma, na imeomba polisi kusaidia kukabiliana nao la sivyo imeonya haitakuwa na budi ila kuchukua sheria mikononi. Tumearifiwa kuwa kuna askari wanaoshirikiana na wahuni, na hii ina maana kuwa baadhi ya maafisa wetu WA NGAO au polisi wanaunga mkono uhalifu,” akasema.

Kulingana na kamishna, karibu vijana 300 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa Confirm, Mauki, Watizedi na Mungiki wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.

Katika juhudi za kukabiliana na uhalifu, Bw Kibara alitangaza kuwa wamefanya mabadiliko makubwa kwa kumteua  OCS mgeni katika kituo cha Polisi cha Rhonda.

Alibaini  kuwa kuna mipango ya kubadilisha maafisa wa polisi katika maeneo yaliyotajwa kuwa hatari kwani wengi wao wamefanya kazi kwa vituo hivyo kwa muda mrefu na kufanya urafiki na wahalifu.

Afisa huyo aliongeza kuwa pia watafanya mabadiliko ya viongozi wote wa Mpango wa Nyumba Kumi kwa sababu wakaazi wengi wameonyesha kutokuwa na imani na kususia kupeana taarifa kwa hofu ya kushambuliwa na magenge hayo.

Kulingana na Bw Kibara, wanachama watatu wa magenge hayo wameuawa katika mashambulizi ya kulipiza kisasi miongoni mwao baada ya mshukiwa wa kiongozi wa genge la Mauki kuuawa.

Kamanda wa polisi Zachary Kimani kwa upande wake, alitoa hakikisho kupambana na uhalifu.

  • Tags

You can share this post!

Majina yaliyopendekezwa kutwaa nafasi ya Kadhi Mkuu yapingwa

Idadi ya waliothibitishwa kufariki Shakahola sasa yagonga...

T L