• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Makabiliano Sudan watu zaidi ya 50 wakiuawa

Makabiliano Sudan watu zaidi ya 50 wakiuawa

NA MASHIRIKA

KHARTOUM, SUDAN

SAUTI za milipuko ya risasi jana ziliendelea kusikika kwa siku ya pili katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, huku madaktari nchini humo wakisema kuwa jumla ya watu 56 wameuawa tangu mapigano kuzuka baina ya vikosi tofauti vya jeshi.

Mapigano hayo yaliendelea huku Amerika, Saudi Arabia na Milki ya Kiarabu (UAE) zikizirai pande zinazozozana “kumaliza mapigano hayo mara moja bila masharti yoyote”. Walioshuhudia walisema kuwa kando na Khartoum, milio ya risasi na makombora ilisikika katika miji ya Omdurman na Bahri. Vituo kadhaa vya televisheni vilionyesha moshi ukifuka kutoka sehemu tofauti za Khartoum.

Chama cha Kitaifa cha Madaktari cha Sudan kilisema kuwa jumla ya watu 56 wameuawa huku wengine 595 wakijumuisha wanajeshi wakijeruhiwa vibaya tangu mapigano hayo kuanza baina ya jeshi na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) kuzuka mnamo Jumamosi.

Vikosi hivvyo vimekuwa viking’ang’ania mamlaka huku makundi tofauti yakiendelea kujadiliana kuhusu mchakato wa kubuni serikali ya mpito tangu mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika 2021.

Taharuki hiyo inatokana na hali ya kutoelewana baina ya jeshi, linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na RSF, linaloongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo kuhusu vile vikosi vya waasi vinafaa kujumuishwa katika jeshi la kitaifa na upande unaofaa kusimamia mchakato huo.

Wanahabari walio katika jiji la Khartoum walisema kuwa hali katika jiji hilo ni tete. Wakazi wengi wamejipata katikati mwa mapigano hayo.

“Hali hii haionekani kutulia hata kidogo,” wakaeleza wanahabari.

“Tayari, jeshi lishatoa taarifa likisema kuwa halitafanya mashauriano yoyote na Rapid Support Forces (RSF) hadi pale vikosi hivyo vitasambaratishwa na makundi ya wanamgambo kukabiliwa vilivyo.”

“Tunaendelea kushuhudia mapigano jijini Khartoum karibu na Ikulu ya Rais,” akaeleza mkazi mmoja.

“Tunaweza kusikia milio ya risasi. Tunasikia milio ya makombora pia. Ingali kubainika anayedhibiti Ikulu, kwani kuna makabiliano yanayoendelea kuhusu udhibiti wa kituo cha televisheni cha serikali. Jeshi linasema limechukua udhibiti wake na pia Uwanja wa Kitaifa wa Ndege wa Khartoum.” Mataifa yenye ushawishi duniani—Amerika, Urusi, Misri, Saudi Arabia, Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU)—yameomba kusitishwa kwa makabiliano hayo.

Kwenye taarifa, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Amerika Anthony Blinken, alisema kuwa amezungumza na mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Saudi Arabia na UAE, ambapo walikubali kuwa “ni muhimu” mapigano hayo kusitishwa mara moja.

“Ninamrai Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman al-Burhan na Jenerali Mohamed Hamdan Degalo kuchukua hatua kupunguza taharuki na usalama wa raia wote,” akasema.

“Njia ya pekee ni kurejea kwa mashauriano yanayounga mkono demokrasia na matakwa ya watu wa Sudan.”

  • Tags

You can share this post!

BORESHA AFYA: Fahamu umuhimu wa cheri

TAHARIRI: Ni makosa kwa IG Koome kujibizana na wanasiasa

T L