• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mashauri yaanza DRC, M23 washambulia zaidi

Mashauri yaanza DRC, M23 washambulia zaidi

KINSHASA, DRC

MAZUNGUMZO yanaendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kusuluhisha mvutano wa kidiplomasia baina yake na Rwanda.

Mazungumzo hayo pia yanalenga kukomesha mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea mashariki mwa taifa hilo.

Mazungumzo hayo yaliyoanza jana yanaongozwa na Rais Joao Laurenco wa Angola na rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Hilo linafuatia mkutano kati ya viongozi hao wawili na Rais Paul Kagame wa Rwanda mnamo Ijumaa wiki iliyopia.

Rais Kagame amekanusha madai ya kuunga mkono kundi la waasi la M23, ambalo majuzi lilianza mashambulio mapya yaliyosababisha maafa makubwa kwa raia.

Viongozi hao wawili pia wanatarajiwa kuzungumza na waathiriwa wa vita hivyo.

Serikali ya taifa hilo inatarajiwa kukutana na wawakilishi wa makundi tofauti yaliyojihami katika jiji kuu la Kenya, Nairobi wiki ijayo.

Mazungumzo hayo ni sehemu ya juhudi ambazo zimekuwa zikiendeshwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kurejesha amani nchini humo.

Siku moja baada ya wanajeshi wa Kenya kuwasili mjini Goma katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Bw Kenyatta aliwasili jijini Kinshasa alikopangiwa kukaa kwa siku mbili.

Kiongozi huyo ameandamana na Katibu Mkuu wa EAC, Peter Mathuki.Bw Kenyatta amepangiwa kukutana na Rais Felix Tshisekedi jijini Kinshasa.

“Rais mstaafu wa Kenya pia atakutana na marais wa mabunge, maafisa wa serikali, wanadiplomasia, wawakilishi wa jamii, viongozi wa kidini, machifu wa kitamaduni na viongozi wa vyama vya wanawake kutoka mikoa ya Ituri, Kivu Kusini na Kivu Kaskazini, ambao wamesafiri Kinshasa ili kukutana na kujadiliana na Bw Kenyatta,” ikaeleza taarifa kutoka kwa afisi ya Rais Tshisekedi.

Washauri wa baraza kuu la viongozi wa EAC na Rais Evariste Ndayishime wa Burundi pia wamealikwa kushiriki kwenye mazungumzo hayo.

Mazungumzo ya Kinshasa yanajiri wiki moja baada ya mkutano mwingine wa ngazi za juu uliofanyika jijini Sharm El Sheikh, Misri, kati ya marais Ndayishimiye, Kagame na William Ruto wa Kenya.

Mnamo Ijumaa wiki iliyopita, wapiganaji wa kundi la M23 walikabiliana vikali na wanajeshi wa serikali ya DRC mkoani Kivu Kaskazini.

Wakazi wa maeneo ya Rugari na Rutshuru waliripoti kuwepo kwa mapigano makali.Mapema wiki iliyopta, jeshi la DRC lilisema limeanza kushambulia kwa mabomu maeneo ya waasi hao kwa kutumia ndege aina ya Sukhoi-25 pamoja na helikopta aina ya Mi-24.

Wapiganaji wengi wa M23 ni wa asili ya kabila la Tutsi.

Kufuatia mashambulio hayo, maelfu ya wakazi wamelazimika kutoroka makwao na kukimbilia maeneo salama.

  • Tags

You can share this post!

Ronaldo adai kusalitiwa na Man-Utd, afichua mpango wa...

Wajenzi wapata kaburi la halaiki la zamani shuleni

T L