• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Ronaldo adai kusalitiwa na Man-Utd, afichua mpango wa kujiendea zake

Ronaldo adai kusalitiwa na Man-Utd, afichua mpango wa kujiendea zake

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo, 37, amedai “kusalitiwa” na waajiri wake Manchester United na kufichua kwamba hana heshima kabisa kwa mkufunzi Erik ten Hag ambaye ni miongoni mwa vinara watatu wakuu wanaomsukuma nje ya Old Trafford.

Mnamo Agosti 2022, Mreno huyo aliahidi kuanika anachokipitia kambini mwa Man-United baada ya jaribio lake kuondoka Old Trafford ili achezee kikosi kinachoshiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu kugonga ukuta.

Katika mahojiano yake na Piers Morgan wa TalkTV yaliyochapishwa na gazeti la The Sun, Ronaldo anahisi kuwa hakuna “mabadiliko muhimu” ambayo yamefanywa na Man-United tangu kocha Alex Ferguson astaafu mwaka wa 2013.

Aidha, anahisi kuwa mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) “hawakumuonea huruma wala kusimama naye” mwanawe mmoja alipoaga dunia mnamo Aprili kabla ya mwingine mdogo kuugua na kulazwa hospitalini mwezi Julai.

Anakerwa pia na mazoea ya waliokuwa wachezaji wenzake kambini mwa Man-United kumkosoa huku akisisitiza kuwa baadhi yao, akiwemo Wayne Rooney, “wanaomuonea wivu” kutokana na mafanikio yake ugani.

Man-United walipepeta Fulham 2-1 katika gozi la EPL mnamo Jumapili ugani Craven Cottage na kusalia katika nafasi ya tano jedwalini kwa alama 26. Wameshinda mechi nane, kupiga sare mbili na kupoteza michuano minne kati ya 14 ya muhula huu chini ya Ten Hag aliyetokea Ajax ya Uholanzi msimu jana.

Kutokana na ugonjwa ambao haujabainishwa, Ronaldo hajachezea waajiri wake tangu wapigwe 3-1 na Aston Villa mnamo Novemba 6 katika pambano la EPL lililomshuhudia akivalia utepe wa nahodha.

Ten Hag alimwacha Ronaldo nje ya kikosi kilichovaana na Chelsea mwezi uliopita, siku tatu baada ya kukataa kutokea benchi na kucheza dhidi ya Tottenham Hotspur.

“Simheshimu Ten Hag kwa sababu ananidharau. Suala la heshima ni la nipe nikupe,” akasema Ronaldo alirejea Man-United mwanzoni mwa msimu wa 2021-22 baada ya kuagana na Juventus waliomsajili kutoka Real kwa mkataba wa miaka minne.

Licha ya Ronaldo kuibuka mfungaji bora ugani Old Trafford muhula uliopita na kuambulia nafasi ya tatu kwenye orodha ya wafungaji bora wa EPL kwa mabao 18, matokeo ya Man-United yalikuwa ya kufadhaisha.

Walikosa kufuzu kwa soka ya UEFA baada ya kutupwa katika nafasi ya sita ligini kwa alama 58 – idadi ndogo zaidi ya pointi katika historia yao tangu wajizolee alama 59 mnamo 1990-91.

Kwa mujibu wa magazeti mengi Uingereza, kusakata kabumbu ya Europa League msimu huu ni jambo ambalo Ronaldo anayewaniwa upya na Sporting Lisbon ya Ureno anahisi limemdunisha ikizingatiwa hadhi yake katika ulingo wa soka.

“Ronaldo ni mshindi mara tano wa Ballon d’Or. Kuna klabu kubwa ambazo ziko tayari kuweka mezani ofa nono ili kujivunia maarifa yake katika UEFA,” likasema gazeti la Mirror Sport.

“Ronaldo angali katika ubora wake na mashabiki wana kila sababu ya kutarajia makuu kutoka kwake. Ana kiu ya kusakata UEFA na kustaafu soka akivalia jezi za kikosi cha haiba,” likasisitiza gazeti la The Sun.

Mbali na Real, AS Roma, Bayern Munich na Paris Saint-Germain (PSG) klabu nyingine inayomezea mate huduma za Ronaldo ni Chelsea iliyo radhi kutoa ofa ya Sh10.2 bilioni ili kumshawishi kutua Stamford Bridge.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Namwamba asema wachezaji wa Ligi Kuu Kenya wanastahili...

Mashauri yaanza DRC, M23 washambulia zaidi

T L