• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 5:50 AM
Matumaini meli ya kwanza Ukraine ikisafirisha nafaka

Matumaini meli ya kwanza Ukraine ikisafirisha nafaka

NA MASHIRIKA

ODESSA, UKRAINE

MELI ya kwanza iliyobeba nafaka jana iliondoka katika bandari ya Odsesa nchini Ukraine, chini ya mkataba maalum kati yake na Urusi.

Maafisa wa serikali za Uturuki na Ukraine walisema meli hiyo iliondoka kwenye bandari huyo jana asubuhi.

Urusi imekuwa ikizuia shughuli zozote kuendelea katika bandari za Ukraine tangu Februari, ijapokuwa mataifa hayo mawili yamekubaliana kuruhusu shughuli za usafiri na uchukuzi wa meli kurejelewa.

Wadadisi wanasema huenda utekelezaji wa mkataba huo ukapunguza mzozo wa chakula unaoshuhudiwa kote duniani. Hilo pia linatarajiwa kupunguza bei za bidhaa za matumizi ya msingi kama vile mafuta.

Kwenye taarifa iliyotolewa kabla ya meli hiyo kuondoka, Uturuki ilisema kuwa, meli hiyo ambayo inaelekea nchini Sierra Leone, itapitia nchini Lebanon.

Iliongeza kuwa, meli nyingine zimepangiwa kuondoka na kuelekea katika sehemu tofauti duniani, majuma kadhaa yajayo.

Kamati ya Pamoja ya Kutekeleza Mpango huo (JCC), ilisema kuwa meli hiyo inabeba tani 26,000 za mahindi, na inatarajiwa kuwasili leo nchini Uturuki ili kukaguliwa.

“Leo (jana Jumatatu), Ukraine na washirika wake wamechukua hatua muhimu kudhibiti hali ya ukosefu wa chakula duniani,” akasema Waziri wa Miundomsingi wa Ukraine, Alexander Kubrakov.

“Kufunguliwa tena kwa bandari kutatuzalishia Sh100 bilioni kutokana na mauzo ya nafaka. Ni hali ambayo pia itatupa nafasi ya kupanga sekta ya kilimo mwaka 2023,” akasema.

Waziri huyo aliongeza kuwa, meli nyingine 16 zimepangiwa kuondoka kwenye bandari zilizo katika eneo la Odesa.Ilichukua miezi miwili kubuni mkataba huo, ambao unatarajiwa kutekelezwa kwa siku 120 zijazo.

Shughuli za kubuni mkataba huo ziliendeshwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwa ushirikiano na Uturuki.

Mkataba unaweza kuanza kutekelezwa upya ikiwa pande husika zitakubali.Hatua ya Urusi kufunga bandari za Ukraine imesababisha mzozo wa chakula duniani, hasa upungufu wa bidhaa kama ngano, mafuta na mbolea.

Chini ya mkataba huo, Urusi imekubali kutozishambulia bandari wakati meli zinasafirisha chakula.Kwa upande wake, Ukraine imekubali kuwa meli zake za kijeshi zitatoa mwongozo wa meli zitakazokuwa zikisafirisha chakula.

Uturuki ndiyo imepewa jukumu la kuziangalia na kuzikagua meli hizo, chini ya usaidizi wa UN. Hatua hiyo inalenga kuondoa tashwishi ya Urusi kwamba baadhi ya meli hizo zinatumiwa kusafirisha silaha za vita.

Bandari tatu nchini Ukraine—Odesa, Chornomorsk na Pivdenny— ndizo zinatarajiwa kutumika pakubwa kusafirisha bidhaa hizo.

Hata hivyo, tashwishi ilizuka kuhusu utekelezaji wa mkataba huo baada ya Urusi kurusha makombora mawili hatari katika bandari ya Odessa mara tu baada ya kufikiwa kwake.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema kuwa Urusi haiwezi kuaminiwa kuzingatia makubaliano ya mkataba huo.Wakati huo huo, mmoja wa wafanyabiashara tajiri zaidi nchini Ukraine aliuawa jana baada ya shambulio lililotekelezwa na vikosi vya Urusi katika mji wa Mykolaiv.

  • Tags

You can share this post!

Majonzi ndugu 2 waliouawa kikatili wakikumbukwa

Shangwe na hoihoi Lee Njiru akizindua kitabu kuhusu ikulu

T L