• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Miili 440 yapatikana kwenye kaburi Ukraine

Miili 440 yapatikana kwenye kaburi Ukraine

NA MASHIRIKA

KYIV/KUPIANSK, Ukraine

MAAFISA wa serikali ya Ukraine wamepata miili 440 ikiwa imezikwa katika kaburi moja la pamoja katika mji mmoja kaskazini mwa nchi hiyo uliokombolewa kutoka kwa wanajeshi wa Urusi.

Maafisa hao walisema kupatikana kwa miili hiyo, ni ithibati ya uhalifu wa kivita uliotekelezwa na wavamizi waliodhibiti eneo hilo kwa miezi kadha.

“Urusi imetekeleza mauaji ya kinyama kila mahali na sharti iadhibiwe kwa hilo,” Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, alisema katika hotuba aliyotoa kupitia video usiku wa kuamkia Ijumaa.

Kaburi hilo la halaiki, ambalo liligunduliwa katika mji wa Izium ambao ulikuwa umedhibitiwa na Urusi, ndilo kubwa zaidi bara Uropa tangu kutokea kwa vita vya Balkan katika miaka 1990s.

Wanajeshi walikomboa Izium baada ya maelfu wa wanajeshi wa Urusi kutoroka eneo hilo na kuacha bunduki nyingi na risasi.

“Kwa miezi kadha, dhuluma, mateso na mauaji ya halaiki yalitekelezwa katika maeneo yaliyodhibitiwa na wanajeshi wa Urusi,” mshauri wa Zelenskiy, Mykhailo Podolyak akasema kupitia ujumbe wa Twitter.

“Kila mtu anataka vita vikomeshwe badala ya makombora kutumwa. Hatuwezi kuwaacha watu wetu waangamizwe na mashetani,” Podolyak akaongeza.

Urusi haikutoa taarifa yoyote kuhusu kupatikana kwa kaburi la halaiki.

Awali, nchi hiyo ilikana madai ya wanajeshi wake kutekeleza vitendo vya ukiukaji haki baada ya kuvamia Ukraine mnamo Februari 24.

Ilitaja operesheni ya wanajeshi wake katika taifa hilo kama “operesheni maalum ya kijeshi” ya kuwapokonya Ukraine silaha za maangamizi.

Wanajeshi wa Ukraine pia walikomboa mji wa Kupiansk, ulioko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Mji huo ulioko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ulisalia mahame baada ya wanajeshi wa Urusi, kuachilia kituo kimoja cha polisi walichokuwa wamekiteka.

Bendera ya Urusi na picha za Rais Vladimir Putin zilitapakaa sakafuni pamoja na vioo vilivyovunjika.Rekodi zote ziliteketezwa.

Milango ya seli za kituo hicho ilikuwa na alama za damu pamoja na magodoro.

“Hakuna umeme na simu za rununu. Kama kungekuwa na stima, angalau tungeweza kutizama runinga. Iwapo tungekuwa na simu, tungewasiliana na jamaa zetu,” afisa mmoja katika kituo hicho cha polisi alisema.

Baada ya kukomboa maeneo kadhaa kaskazini wa Ukraine, wanajeshi wa nchi hiyo, walisema kuwa wamepata motisha ya kukomboa maeneo mengine yanayodhibitiwa na Urusi.

Walisema wanajeshi wa Urusi wamegura eneo la Kharkiv na wanajiandaa kupigania mikoa jirani ya Luhansk na Donetsk.

“Bila shaka inatia moyo kwamba wanajeshi wa Ukraine wamefaulu kukomboa maeneo makubwa ya Ukraine kutoka kwa udhibiti wa Urusi,” akasema Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg.

“Vile vile, tungetaka kuelewa kuwa hii sio mwanzo wa mwisho wa vita. Sharti tujiandae kwa wajibu mkubwa,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Ruto atimize ahadi alizotoa kwa wanawake...

Wandani wa Uhuru wajaa hofu katika serikali ya Ruto

T L