• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:09 PM
Mkosoaji wa Kagame atupwa jela miaka 7

Mkosoaji wa Kagame atupwa jela miaka 7

Na MASHIRIKA

KIGALI, Rwanda

MWANAHARAKATI ambaye amekuwa akitumia mtandao wa Youtube kuikosoa serikali, Dieudonne Niyonsenga, jana alihukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani kwa kudhalilisha maafisa wa serikali.

Niyonsenga, ndiye mkosoaji wa hivi karibuni wa serikali mwenye wafuasi wengi kwenye Youtube, kutupwa gerezani katika taifa hilo la Afrika Mashariki linalodhibiti vikali matumizi ya intaneti.Wakili wake Gatera Gashabana amesema kwamba watakata rufaa kupinga hukumu hiyo dhidi ya Niyonsenga.

Mwanaharakati huyo anaendesha akaunti ya Youtube inayojulikana kwa jina Ishema TV, iliyo na zaidi ya wafuasi milioni 15. Alipatikana na hatia ya kuwadhalilisha maafisa wa serikali.“Mahakama imebaini kuwa mshtakiwa alitekeleza makosa hayo kimakusudi,” akasema jaji.

Niyonsenga ambaye alihukumiwa bila kuwepo mahakamani, pia alitozwa faini ya Sh490,000.Mahakama iliagiza, Niyonseng akamatwe mara moja na apelekwe gerezani aanze kutumikia kifungo chake.

Niyonsenga alihukumiwa adhabu hiyo mwezi mmoja baada ya Yvonne Idamange – mkosoaji mkubwa wa Rais Paul Kagame – kufungwa jela miaka 15.Idamange, 42, alijizolea umaarufu mkubwa kutokana na video zake kupitia mtandao wa Youtube.

Alipatikana na makosa sita, ikiwemo uchochezi wa ghasia na uasi, kupuuza kumbukumbu za mauaji ya kimbari, kueneza habari za uzushi na kuchochea vurugu.Upande wa mashtaka uliambia korti kwamba Idamange alitumia mtandao wa Youtube kukosea heshima Rais Kagame na serikali kwa kudai kuwa yeye ni dikteta.

Mahakama pia iliambiwa kwamba Idamange alidai kwamba maafisa wa serikali ya Rais Kagame walitumia mauaji ya halaiki ya 1994 kwa maslahi yao ya kibinafsi kwa kugeuza eneo la kumbukumbu ya mauaji kuwa kivutio kwa watalii.

Idamange ambaye mtandao wake wa Youtube una wafuasi 18,900, amekuwa akishikilia kuwa yeye ni miongoni mwa waathiriwa wa mauaji hayo.Kulingana na Umoja wa Mataifa (UN), mauaji hayo yalisababisha vifo vya watu 800,000.

Idamange pia alidaiwa kwa kumpiga na kumjeruhi afisa wa polisi wakati wa kukamatwa kwake.Mbali na kifungo cha miaka 15 jela, alipigwa faini ya Sh2 milioni. Awali,upande wa mashtaka ulipendekeza miaka 30 jela na faini ya Sh600,000.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Right Watch, lilizungumzia wasiwasi wake mnamo Machi, mwaka huu, kuhusu kuongezeka kwa visa vya kukamatwa na kushtakiwa kwa watu wanaokosoa mamlaka za Rwanda kwenye mitandao ya kijamii.

Shirika hilo lilikumbusha kauli ya vitisho ya Rais Kagame ya mwaka 2019, aliposema:’ Wale mnaowasikia wakizungumza mitandaoni, wapo Amerika, Afrika ya Kusini au Ufaransa. Kwa sababu wapo mbali, Wanafkiri wapo kwenye usalama.

Lakini wapo karibu na moto, na siku watakapoukaribia, basi moto utawaunguza.”Rais Kagame ambaye amekuwa akiongoza Rwanda tangu kumalizika kwa mauaji ya halaiki ya 1994, amekuwa akikosolewa mara kwa mara kwa kuwakandamiza wapinzani na kuuminya uhuru wa kujieleza.

You can share this post!

Vipusa wa Chelsea waponda Servette ya Uswisi bila huruma...

Raia wa kigeni wanaswa msakoni Addis Ababa

T L