• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Mmiliki wa shamba Afrika Kusini ashtakiwa kwa kumpiga risasi mwanamke mweusi

Mmiliki wa shamba Afrika Kusini ashtakiwa kwa kumpiga risasi mwanamke mweusi

Na AFP

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

RAIA mmoja wa Afrika Kusini, ambaye ni mweupe alifikishwa mahakamani mnamo Alhamisi kwa kosa la kumpiga risasi na kumjeruhi mwanamke mmoja mweusi akidai alidhani mama huyo ni kiboko.

Polisi walisema kuwa, Paul Hendrik van Zyl, 76, alifikishwa mahakamani Alhamisi kwa kumpiga risasi mama huyo ambaye alikuwa akivua samaki pamoja na mwenzake katika mji wa Lephalale, kaskazini mwa mkoa wa Limpopo.

Kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kuendesha Mashtaka (NPA), Hendrik anakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuua kwa kukusudia.

“Mshukiwa aliyekamatwa alidai kuwa alikuwa akiwapiga risasi wanyama aina ya kiboko,” msemaji wa polisi, Mamphaswa Seabi akasema kwenye taarifa.

Mwanamke huyo, Ramokone Linah, mwenye umri wa miaka 38, alipata majeraha ya risasi katika mkono wake wa kulia.

“Hata hivyo, mwenzake hajeruhiwa baada ya kujificha,” polisi wakasema.

“Mshtakiwa ni mmiliki wa shamba ambako kisa hicho kilitokea,” akasema Mashudu Malabi-Dzhangi, ambaye ni msemaji wa polisi katika mkoa huo wa Limpopo.

Hendrik aliachiliwa huru kwa dhamana ya dola 62 (sawa na Sh7,130) na kesi hiyo ikaahirishwa ili kutoa nafasi kwa uchunguzi zaidi kuendeshwa kuhusu kisa hicho.

Kesi hiyo itatajwa mnamo Mei 18, mwaka huu.

Nje ya mahakama hiyo, wafuasi wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF), chake mwanaharakati Julius Malema, walifanya maandamano wakipinga dhamana hiyo wakisema ni ya chini mno.

Walidai kuwa dhamana hiyo ilikuwa ndogo zaidi ikizingatiwa kuwa Hendrik alijaribu kumuua mama huyo.

Matukio sawa na hayo huibua kero kubwa nchini Afrika Kusini ambako ubaguzi wa rangi ungali unashuhudiwa miaka 28 baada ya utawala wa dhalimu wa wazungu kufika kikomo.

Katika baadhi ya maeneo nchini humo, Waafrika weusi hawaruhusiwi kutangamana na wenzao weupe kama ilivyokuwa enzi zile za utawala wa ubaguzi wa rangi.

  • Tags

You can share this post!

Presha City ikizuru Leeds, Liverpool ikivizia Newcastle

Kalonzo motoni kusukuma Sonko

T L