• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Kalonzo motoni kusukuma Sonko

Kalonzo motoni kusukuma Sonko

NA WINNIE ATIENO

KIONGOZI WA chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, anazidi kulaumiwa na wanasiasa Mombasa kwa kumruhusu aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko kuwania ugavana katika kaunti hiyo hapo Agosti 9.

Wakiongozwa na aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, viongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) walisema hatua ya Wiper kumpa Bw Sonko tikiti ya moja kwa moja ni kejeli kwa Wapwani.

Bw Omar ambaye ni miongoni mwa wawaniaji wa ugavana wa Mombasa aliwasihi wakazi kuchagua viongozi wenye maadili.

Alisema Bw Sonko hafai kuwania siasa za Mombasa baada ya kubanduliwa na bunge la Kaunti ya Nairobi mwaka wa 2020.

“Ninataka kumwambia Bw Musyoka asitukejeli na kutuchagulia viongozi. Unatuchagulia mtu ambaye anavaa nyororo na bangili kuanzia kichwa hadi miguu sababu watufikiria sisi ni mazuzu! Watu walitudharau sana na kutudhulumu kwa miaka na mikaka, wakatuita wavivu, mazuzu, wakasema pia twapenda starehe na kazi yetu ni kungojea nazi zianguke,” alisema Bw Omar.

Aliwasihi wapigakura kuwaangusha viongozi wote wa Wiper wanaowania viti vya siasa Mombasa.

“Bw Sonko alibandiliwa Nairobi lakini Bw Musyoka anaona anafaa Mombasa? Wacheni madharau,” alisema Ijumaa wakati wa Ifthar na waumini wa Kiislamu katika ukumbi wa Jubilee, Mombasa.

Naye mbunge wa Msambweni, Bw Feisal Bader aliwasihi wapwani kusimama kidete na kutokubali kuchaguliwa viongozi.

Mapema wiki hii, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alidai kuwa Bw Musyoka alimshurutisha Bw Sonko kuwania ugavana Mombasa ili kuharibu kura za mgombea urais wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga.

Kwenye mahojiano na runinga moja, Bw Sonko alisema alipania kuwania kiti chake cha Nairobi lakini akaambiwa na Bw Musyoka kutathubutu.

“Bw Musyoka ndiye aliyezua uamuzi wa mimi kugombea kiti cha Mombasa. Aliniambia jijini Nairobi nitakabiliwa na vita vikali na sababu ninamheshimu nikaungama. Sikukataliwa na wakazi wa Nairobi lakini serikali ndiyo iliyoniondoa,” akasema Sonko.

Hata hivyo, Bw Nassir alimuonya Bw Musyoka dhidi ya kusambaratisha muungano wa Azimio.

“Acha kuingilia siasa za Mombasa kwa kumsukuma Bw Sonko Mombasa. Mwezi mmoja hivi uliopita nilisafiri na Bw Sonko na hakunieleza kuwa ananuia kugombania kiti hiki. Lakini juzi alitangaza kuwa ni Bw Musyoka aliyemshurutisha kunyemelea siasa za Mombasa. Kama ana haja sana na Mombasa, si angekuja mwenyewe?” Mbona atumane,” alisema Bw Nassir.

Bw Musyoka alimshawishi Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo kuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko kwenye uchaguzi wa ugavana akisema ushirikiano huo utapelekea chama cha Wiper ushindi.

Mbunge huyo wa Kisauni aliahidiwa asilimia 60 ya uongozi wa kaunti ya Mombasa endapo watashinda katika makubaliano uliosimamiwa na Bw Musyoka ambapo Bw Sonko alipewa tikiti ya kuwania ugavana.

Wengine wanaogombania ugavana ni pamoja na naibu gavana Dkt William Kingi (Pamoja African Alliance), na aliyekuwa mbunge wa Nyali Bw Hezron Awiti (VDP).

  • Tags

You can share this post!

Mmiliki wa shamba Afrika Kusini ashtakiwa kwa kumpiga...

Kingi asema ameanza harakati ya kujiondoa katika Azimio

T L