• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Mwanamke mwenye ndevu asimulia jinsi alivyojikubali

Mwanamke mwenye ndevu asimulia jinsi alivyojikubali

Na MASHIRIKA

MWANAMKE mmoja aliyekataa kunyoa ndevu zake anaendelea na maisha yake kama kawaida licha ya kudhulumiwa kwa miaka mingi na watu anaokutana nao.

Kwenye makala yaliyochapishwa mara ya kwanza na gazeti la Daily Mail nchini Uingereza, Klyde Warren, 27, kutoka jimbo la Nebraska nchini Marekani, anasema kuwa huwa haruhusu matamshi mabaya kutoka kwa watu – ambao humwambia “anachukiza”- kumzuia kupenda masharubu yake.

Anasisitiza nywele hizo ni miongoni mwa vitu anavyopenda zaidi katika maumbile yake.

Klyde ambaye ni mwanahabari wa kujitegemea, huwa anakejeliwa kwenye appu za mahusiano ya kimapenzi kwa sababu ya ndevu zake. Lakini anasema kamwe hajakata tamaa ya kupata mpenzi anayependa masharubu kwenye uso wake, sawa na anavyoyapenda.

Kiini

Kiini cha kumea nywele nyingi kupindukia kwenye uso wa Klyde bado hakijagunduliwa, lakini licha ya kuathiri mahusiano yake ya kimapenzi, anasema amejifunza kupenda maumbile yake asilia na hivyo matamshi mabaya kutoka kwa watu wengine hayamwathiri.

“Huwa ninakodolewa macho sana na watu kwenye mtandao wa kijamii wa kusaka wapenzi, Tinder, huwa hawapotezi nafasi ya kunitumia jumbe wakinieleza ninavyosinya na kuchukiza,”

“Huwa hainiathiri wakati huo, ninajiamini sana. Hakuna anayependa jumbe kama hizo,” anasema Klyde.

“Baadhi ya watu ninaochumbiana nao huwa wanazikubali nywele zangu vilevile na kuziona kama maumbile yangu ya kipekee, aliyekuwa mpenzi wangu aliniunga mkono sana na alipenda masharubu yake kwa njia mwafaka,” anaeleza.

Klyde aligundua kuwa na masharubu makubwa kwenye uso wake kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 15 na papo hapo akaamua kuacha maumbile yachukue mkondo wake na kuachana na wembe.

Anasema ndevu zake ni rahisi kusafisha na huhitaji tu kunyolewa mara kwa mara na kuoshwa mara moja kwa siku.

“Zilianza nikiwa shuleni na nilikuwa na masharubu makubwa kushinda maumbile ya kawaida. Niliamua tu kuyakubali moja kwa moja,”

“Mamangu alikuwa na la kusema kuhusu uamuzi huo. Hakuzipenda kamwe na akaniambia nizifiche lakini sikujali. Nilikataa kunyoa. Nilijifunza tu kuwa jasiri. Ni sawa kuwa tofauti,”

“Watu wengi hujishuku maumbile yao lakini unapaswa kujifunza kujikubali jinsi ulivyo jambo ambalo si rahisi kabisa. Maumbile yalitaka iwe hivyo basi nitayaamini,” anasema.

Hirsutism ni hali inayosababisha wanawake kuwa na nywele nyingi zinazokua kwenye uso, shingo, kifua, tumbo, sehemu ya chini ya mgongo, makalio au mapaja.

Hali hiyo aghalabu husababishwa na mabadiliko katika viwango vya homoni na kuongezeka kwa homoni za kiume zinazofahamika kama androgens.

Kiini kinachofahamika zaidi cha matatizo hayo ni ugonjwa unaojulikana kama polycystic ovary syndrome (PCOS), uliosababisha hali hiyo kwa Alma Torres, 27, anayeishi Bronx, New York.

Alipata (PCOS) akiwa na umri wa miaka 15, iliyomfanya kumea masharubu usoni mwake.

Baada ya miaka minane ya kunyoa, kutumia nta na kemikali kuziondoa, aliamua kuacha zimee kabisa kama ndevu.

Akizungumza mwaka jana, Alma aliasi kinyozi miaka minne iliyopita na kukubali ndevu zake asilia ambapo sasa anatumia kisa chake kuwatia moyo wengine.

Alipokuwa kijana chipukizi, Alma alijipata akimea shungi kubwa la nywele za uso na akanyoa kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 16 baada ya kudhihakiwa na wanafunzi wenzake darasani.

Alisherehekea miaka minne ya kuadhimisha siku aliyoamua kuacha ndevu zake kukua kwa njia asilia.

Anasema kuwa sasa amejifunza kupenda mwili wake asilia, hivyo basi maoni mabaya kutoka kwa watu wengine hayamwathiri.

Mwanafunzi wa chuo, Caiopa Jade Marja, 23, kutoka Farmville, Virginia, alikejeliwa vikali kwa sababu ya mashasrubu makubwa yaliyomea kwenye uso wake.

Alitumia siku zake shuleni akijihisi asiyefaa baada ya kudhihakiwa kila mara na wanafunzi wenzake kwa kuwa na “nywele nyingi kupindukia” kiasi kwamba angeficha wembe kila siku ili kunyoa nywele zilizomea kwenye uso na mikono yake.

Aliendelea hivyo hadi 2016, akiwa na umri wa miaka 19, alipogunduliwa kwamba anaugua (PCOS), ugonjwa unaoathiri jinsi mayai ya mwanamke yanavyofanya kazi.

“Ninaugua PCOS, kumaanisha kuwa ninasheheni kiwango cha juu zaidi cha homoni za kiume almaarufu testosterone mwilini mwangu kama mwanamke. Nilidhulumiwa mno kwa kuwa na “nywele nyingi kupindukia”na kumea masharubu usoni,” anasimulia Caiopa.

Athari tatu kuu za PCOS ni hedhi zisizoambatana, kiwango cha juu cha homoni za androgen, na kiwango cha juu cha homoni za kiume mwilini na mayai ya kike yaliyoathiriwa hivyo kuwa makubwa kuliko kawaida.

Caiopa anakumbuka jinsi alivyotumia kemikali za kuondoa nywele kwenye mikono yake na kupitisha wembe kisiri shuleni ili anyoe masharubu yake.

“Ilikuwa inatisha mno nikikumbuka sasa,” anasema.

Mnamo Juni 2019, alianza kugundua kurasa nyingi kwenye mitandao ya kijamii inayoendeshwa na wanawake wengine ‘wenye ndevu’ jambo lililkuwa kuu kwake kwa sababu hakujua kuna jamii zima ya wanawake kama yeye.

Baada ya miaka minane ya kunyoa kila mara, aliamua kuweka kando nyembe zake mnamo Disemba na hajawahi kutazama nyuma tangu hapo.

Mwaka uliopita, shirika la habari la Uingereza, BBC, liliangazia kisa cha Theresia Mumbi, 35, ambaye si mwanamke wa kawaida kutokana na ndevu zake nyingi kama mwanaume.

Mumbi ambaye ni mama wa mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka minane, alikuwa akifanya kazi kama utingo jijini Nairobi, wakati wa mahojiano.

Kulingana naye, alianza kugundua hali yake mnamo 2005 alipomaliza masomo ya sekondari na kuanza kutafuta ajira.

Alisimulia jinsi masharubu yake yalivyoanzas kukua kwa kasi ambapo aliamua kunyoa bila kujua alikuwa anaharibu mambo zaidi kwa sababu, kadri alivyonyoa ndevu zake ndivyo zilivyozidi kukua hata zaidi.

“Nikiwa shuleni nilikuwa na nywele nyingi hata hivyo sikujishughulisha sana kwa sababu nilidhani ni jambo la kawaida,”

“Nilipokamilisha masomo, zilianza kumea kwa kasi na ikabidi nianze kuzinyoa ili nizifiche katika juhudi za kufanana na wanawake wenzangu,” akaeleza.

Nyoa

Alikuwa akinyoa kila wakati ambapo kila mara ndevu zake zilimea kwa kasi na kuongezeka hata zaidi.

Isitoshe, ngozi yake ilianza kuharibika kutokana na kujichubua katika juhudi za kumaliza masharubu kwenye uso wake.

Baada ya kuchoshwa na kuficha maumbile yake asilia kila wakati na kuhofia kuharibu uso wake hata zaidi kwa kujichubua, Mumbi aliamua kutonyoa tena masharubu yake na kujikubali na hapo ndipo masaibu yake yalipoanzia.

Alisimulia jinsi watu walivyoshangazwa na maumbile yake huku wakimkejeli hadharani kiasi cha kumfanya kujifungia nyumbani kwake wakati hakuwa kazini.

“Sikuwa nikitoka nje kabisa hata ningelemewa na njaa kiasi gani. Nilikuwa nikisubiri hadi usiku ili niende sokoni au dukani kununua chakula,”

“Nilijawa na aibu. Niliogopa kusemwa na majirani kwa sababu ya ndevu zangu. Kazini nilikuwa sawa kwa sababu wafanyakazi wenzangu walinielewa,” akaeleza BBC wakati wa mahojiano hayo Januari mwaka jana.

You can share this post!

Rais Suluhu aanza kazi kwa kutumbua majipu

Sossion aililia serikali shule zifunguliwe Mei