• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 AM
Mwili wa Philip kuhamishiwa makaburi ya kifalme baadaye

Mwili wa Philip kuhamishiwa makaburi ya kifalme baadaye

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MWILI wa mume wa Malkia wa Uingereza Elizabeth, Philip, ‘ulipumzishwa’ katika chumba maalumu kilichoko katika Kanisa la St George’s Chapel ndani ya Kasri la Kifalme la Windsor.

Chumba hicho kinachojulikana kama ‘Royal Vault’ kipo takribani futi 15 chini ya kanisa hilo.

Mwili huo hautasalia hapo milele bali utahamishiwa katika makaburi ya Kifalme katika eneo la Makumbusho la King George VI, Malkia Elizabeth, 94, atakapofariki.

Malkia Elizabeth atakapofariki, mwili wa Philip utatolewa katika chumba cha Royal Vault na wawili hao ambao waliishi pamoja kwa miaka 73, watazikwa katika makaburi yanayokaribiana katika Makumbusho ya King George VI.

Wazazi wa Malkia Elizabeth na dada yake Bintimfalme Margaret, walizikwa katika makumbusho hayo.

Baadhi ya wanafamilia wa kifalme, hata hivyo, walizikwa kabisa kwenye chumba hicho kidogo cha Royal Vault. Wafalme watatu, akiwemo George IV and William IV walizikwa kabisa kwenye chumba cha Royal Vault.

Lakini miili ya wengine ilihamishwa baada ya miaka kadhaa na kuzikwa katika makumbusho ya King George VI.

Mwili wa Mfalme George VI aliyefariki 1952 ulihifadhiwa katika chumba cha Royal Vault kwa kipindi cha miaka 17 na baadaye ulihamishwa na ukazikwa katika Makumbusho ya George VI.

Katika misa ya wafu katika kanisa la St George’s, Jumamosi, waombolezaji walivalia barakoa na walikaa mbali na hawakukaribiana kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Wanajeshi zaidi ya 730 walishiriki katika tukio hilo, lakini ni watu 30 tu wa familia ya kifalme waliruhusiwa kuhudhuria ibada kanisani.

Mwanamfalme Philip alifariki katika Kasri la Windsor Aprili 9, akiwa na umri wa miaka 99.

Msafara wa magari kuanzia kwenye kasri hadi kanisani uliongozwa na bendi ya ufalme ya Grenadier Guards, majenerali wa jeshi , na wakuu wa huduma za kijeshi.

Raia wa Uingereza kote nchini humo walinyamaza kwa dakika moja kutoa heshima kwa Philip. Makombora yalifyatuliwa katika maeneo tisa kote nchini humo kuashiria mwanzo na mwisho wa kuwa kimya.

Ndege zilizuiliwa kutua au kupaa kwa dakika sita wakati wa kupumzisha mwili. Hafla zote kuu za michezo ziliahirishwa ili kuepusha mgongano na mazishi.

Makao makuu ya Ufalme ya Buckingham yalisema kuwa mipango ya mazishi ilifanyiwa marekebisho kwa kuzingatia kanuni za wizara ya Afya kuepuka maambukizi ya virusi vya corona.

Kabla ya mazishi, Malkia alitoa kwa umma picha anayopenda aliyopiga akiwa na mumewe Philip mnamo 2003. Wageni 30 katika mazishi hayo walivalia makoti ya kuomboleza na medali.

You can share this post!

Kesi ya mauaji ya Sharon kuanza rasmi, DPP asema

Leicester City walenga historia baada ya kufuzu kwa fainali...