• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 3:09 PM
Leicester City walenga historia baada ya kufuzu kwa fainali ya Kombe la FA

Leicester City walenga historia baada ya kufuzu kwa fainali ya Kombe la FA

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Brendan Rodgers wa Leicester City amesema kikosi chake kina “fursa ya kuandikisha historia” baada ya kukomoa Southampton 1-0 uwanjani Wembley, Uingereza mnamo Jumapili na kufuzu kwa fainali ya Kombe la FA kwa mara ya kwanza tangu 1969.

Bao la pekee na la ushindi lililofungwa na Leicester dhidi ya Southampton lilipachikwa wavuni na fowadi raia wa Nigeria, Kelechi Iheanacho katika dakika ya 55.

Mara ya mwisho kwa Leicester City almaarufu The Foxes kutinga fainali ya kampeni zozote za haiba ni mnamo 2000 ambapo walitia kapuni ufalme wa League Cup baada ya kuzamisha chombo cha Tranmere Rovers kwa mabao 2-1 ugani Wembley.

“Hivyo ndivyo mchuano unavyostahili kuwa – kuunda historia. Nimeaminishwa na mashabiki kuhusu jinsi Kombe la FA lilivyo muhimu katika historia ya Leicester,” akasema Rodgers ambaye anawania fursa ya kushinda taji la kwanza katika soka ya Uingereza licha ya kuongoza Celtic ya Scotland kunyanyua mataji saba chini ya kipindi cha miaka mitatu pekee ya ukocha kambini mwa kikosi hicho.

“Tuna nafasi maridhawa ya kuandikisha historia na kuwapa mashabiki wetu kitu cha kujivunia zaidi msimu huu. Kushinda Chelsea katika fainali ni jambo linalowezekana iwapo tutaendeleza ubabe tuliodhihirisha dhidi ya Southampton,” akaongeza Rodgers.

“Ndoto yangu hatimaye imetimia. Nilikuwa nikitazama fainali zote za Kombe la FA nikiwa mdogo. Sasa ni fahari kubwa kwamba nitakuwa nikicheza fainali ya kipute hicho Mungu akijalia,” akasema Iheanacho aliyekamilisha krosi ya Jamie Vardy dhidi ya Southampton almaarufu The Saints.

Mchuano huo kati ya Leicester na Southampton ilihudhuriwa na takriban mashabiki 4,000, hii ikiwa ni sehemu ya majaribio ya kurejea kwa mashabiki uwanjani baada ya baadhi ya kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona nchini Uingereza kulegezwa.

Idadi kubwa ya mashabiki walioruhusiwa kuhudhuria mechi hiyo walikuwa wakazi wa eneo la Brent, Kaskazini mwa jiji la London ambapo uwanja wa Wembley unapatikana.

Nusu-fainali dhidi ya Southampton ilikuwa ya kwanza kwa Leicester kupiga kwenye Kombe la FA tangu 1982.

Southampton walionekana kuzidiwa maarifa katika takriban kila idara uwanjani huku mafowadi wao wakikosi kabisa kumshughulisha kipa Kasper Schmeichel aliyeelekezewa kombora moja pekee na Ibrahima Diallo.

Leicester kwa sasa watavaana na Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Mei 15 na hiyo itakuwa mara yao ya kwanza kunogesha fainali ya kipute hicho tangu wapokezwe kichapo cha 1-0 kutoka kwa Manchester City miaka 52 iliyopita.

Chelsea walifuzu kwa fainali ya Kombe la FA msimu huu baada ya kubandua Man-City kwa kichapo cha 1-0 mnamo Jumamosi ugani Wembley.

Leicester kwa sasa wanajiandaa kualika West Bromwich Albion katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Aprili 22, 2021 uwanjani King Power huku Southampton wakiwaendea Tottenham Hotspur.

Nusu-fainali dhidi ya Leicester ilikuwa ya 12 kwa Southampton kunogesha kwenye historia ya kipute cha Kombe la FA.

Chini ya Rodgers, Leicester iliwabandua Manchester United kwa kichapo cha 3-1 kwenye robo-fainali baada ya kudengua washindani wao wengine wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Brighton, kwenye raundi ya tano. Awali, Leicester walikuwa wamewang’oa Stoke City na Brentford.

Kwa upande wao, Southampton ya kocha Ralph Hasenhuttl iliwapepeta Shrewsbury Town, Arsenal, Wolverhampton Wanderers na Bournemouth katika safari yao ya kujikatia tiketi ya nusu-fainali ya Kombe la FA muhula huu.

Walishuka dimbani dhidi ya Leicester wakiwania rekodi ya kuwa kikosi cha kwanza baada ya Everton mnamo 1965-66 kuwahi kufuzu kwa fainali ya Kombe la FA bila ya kufungwa bao.

Tangu watawazwe mabingwa wa taji la Football League Trophy mnamo 2010, Southampton wamepoteza sasa kila mojawapo ya mechi tano zilizopita uwanjani Wembley, ikiwemo nusu-fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea mnamo 2018.

Mara ya mwisho kwa Leicester kuingia nusu-fainali za Kombe la FA ni mnamo 1982 ambapo walipepetwa 2-0 na Tottenham waliotawazwa wafalme hatimaye.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mwili wa Philip kuhamishiwa makaburi ya kifalme baadaye

Kipa Courtois awaokoa Real Madrid dhidi ya Getafe kwenye...