• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Njaa kuzidi kuathiri Pembe ya Afrika

Njaa kuzidi kuathiri Pembe ya Afrika

NA MASHIRIKA

GENEVA, USWISI 

NJAA itaendelea kuvamia nchi za Pembe ya Afrika inayojumuisha Kenya, Ethiopia na Somalia utafiti wabaini.

Kulingana na ripoti ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), uhaba wa chakula utaendelea kushuhudiwa katika nchi hizo kufuatia ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa nchi hizo za Pembe ya Afrika inaingia katika msimu wa tano wa mvua kidogo.

Shirika hilo limebaini kuwa utabiri wa hali ya hewa Oktoba-Desemba unaonyesha uwezekano wa ukame mkubwa na joto ya hali ya juu.

Kulingana na utafiti huo, mashirika yanayotoa misaada mbalimbali kwa nchi zinazoathiriwa na njaa na ukame huenda yakalemewa kudhibiti majanga hayo.

Mashirika mbalimbali yamekuwa yakionya kuhusu ukame na athari zake kwa miezi kadhaa ila suluhisho halijapatikana.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa, Guleid Artan alisema kuwa uhaba wa mvua utaendelea kushuhudiwa kwa muda mrefu katika nchi za Pembe ya Afrika.

“Ripoti hiyo inaonyesha kuwa tunaingia msimu wa tano wa mvua kidogo itakayodumu kwa muda mrefu,” akasema Bw Artan.

“Nchini za Ethiopia, Kenya na Somalia ziko katika ukingoni mwa majanga (njaa na ukame) ambayo hayajawahi kutokea,” akaongeza mkurugenzi huyo.

Ukame umesababisha kupanda kwa bei ya vyakula katika nchi mbalimbali.

Kadhalika, kupanda kwa bei ya mafuta duniani kufuatia vita vya Ukraine, kumeathiri nchi kadhaa Afrika.

Mnamo Juni, Benki ya Dunia ilitabiri kuwa huenda watu milioni 66.4 katika eneo la Pembe ya Afrika wataathiriwa na uhaba wa chakula na maji na wakahitaji msaada wa dharura.

Naye msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Carla Drysdale, alisema kuwa shirika hilo liko tayari kuingilia kati ili kuwapa waathiriwa tumaini.

“Shirika la WHO liko tayari kusaidia kwa kuwa ni wakati kama huu ambao waathiriwa hupoteza matumaini. Ni vyema kusimama na nchi zinazopitia hali kama hizo ili wananchi wasipoteze matumaini,” akasema Carla Drysdale.

Takriban Wakenya milioni moja kutoka maeneo kame wanakabiliwa na baa la njaa na uhaba wa maji.

Mamlaka ya Kupambana na Kudhibiti Ukame (NDMA) ilisema kuwa watoto 884,464 ambao wapo chini ya umri wa miaka mitano, na akina mama 115, 725 ambao ni wajawazito, wanakabiliwa na utapiamlo kwa kukosa chakula cha kutosha mwilini.

Janga la ukame pia limeathiriwa ufugaji na kuwalazimisha wafugaji kuhamia maeneo mengine kutafuta malisho.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Magavana wapya wakague madeni ya zamani ili...

Watoto wawili wafa, 19 walazwa baada kula asali yenye sumu

T L