• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Maafisa waonya wakimbizi kutoka TZ kuhusu silaha

Maafisa waonya wakimbizi kutoka TZ kuhusu silaha

NA ROBERT KIPLAGAT

MAAFISA wa usalama katika Kaunti ya Narok wamewaonya wakimbizi kutoka Tanzania wanaotoroka shughuli ya kuwafurusha kikatili katika eneo la Ngorongoro dhidi ya kuingia Kenya wakiwa wamejihami.

Kamishna wa eneo hilo, Isaac Masinde, ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya usalama kaunti hiyo alisema maafisa wa usalama wametumwa kwenye mpaka kati ya Kenya na Tanzania mjini Narok ili kuwakagua wakimbizi.

“Kama Kenya, tuna sheria zetu na tunataka kuhakikisha wanaoingia nchini ni watu wenye nia safi wanaohitaji msaada wa kibinadamu. Hatuwezi kukubali watu wenye nia mbaya,” alisema Bw Masinde.

Msimamizi huyo alisema kulingana na sheria ya kimataifa, hakuna raia wa kigeni atakayenyimwa msaada wa kimatibabu na kibinadamu mradi tu afuate sheria za Kenya.

Alifichua kwamba, kuna Wamaasai karibu 400 raia wa Tanzania ambao wameingia Kenya rasmi na kupokea matibabu katika vituo mbalimbali vya afya nchini.

Alisisitiza kuwa Kenya haijachangia kwa vyovyote yanayoendelea Tanzania akisema anatumai mgogoro huo utasuluhishwa ili wakimbizi waweze kurejea nchini mwao.

“Tunatumai suala hili litatatuliwa haraka na serikali yao ili tuwarejeshe kwa sababu wakizidi kukaa hapa watasababishia Kenya changamoto zaidi,” alisema.

Mwakilishi wa Msalaba Mwekundi Nchini Olposimoru Jackson Mako alisema kuna watu 2500, miongoni mwao watoto 1300 wanaohitaji msaada.

Bw Masinde vilevile aliwaonya vikali wanasiasa wa Kenya dhidi ya kuingilia ufurushaji unaofanyika katika eneo la Ngorongoro nchini Tanzania. “Wanasiasa wa Kenya wanapaswa kujiepusha na suala hili. Hili ni suala linalohusu serikali mbili na hivi punde tatizo hili litatatuliwa,” alisema Bw Masinde.

Msimamizi huyo alionya viongozi wa jamii ya Wamaasai nchini dhidi ya kuchochea wakazi. Siku chache tu zilizopita, wakazi zaidi ya 2,000 katika Hifadhi ya Ngorongoro walikuwa wanaendelea na maisha yao ya kawaida ya ufugaji na utamaduni katika eneo ambalo wameliita nyumbani tangu jadi.

Balaa ilizuka Ijumaa jioni wakati watu katili waliojihami na wanaoaminika kuwa polisi wa Tanzania walipowavamia kwa kuwatandika kinyama huku wengi wakiachwa na majeraha mabaya na baadhi kuripotiwa kuaga dunia.

Pasipo kwingine pa kukimbilia, Wamaasai hao zaidi ya 2500 waliokuwa wakiishi Ngorongoro walitorokea Kenya na sasa wamepiga kambi kwenye mipaka ya Olposimoru na Olturoto katika manyatta za kitamaduni ambapo wamejumuishwa katika jamii za Wamaasai Wakenya.

Hata hivyo, janga la kibinadamu linatokota huku wafugaji hao wakiandamana na mamia ya mifugo yao pamoja na watoto, wakiendelea kufurika nchini.

Baadhi ya wahasiriwa wa ufurushaji huo wa kinyama waliozungumza na Taifa Leo kwenye kambi ya Olposimoru walisimulia kwa majonzi jinsi wanavyokabiliwa na tishio la kupoteza mali, ikiwemo ardhi, mifugo na hata maisha huku wakishangaa iwapo watawahi kurejea nyumbani.

  • Tags

You can share this post!

ULIMBWENDE: Njia za kiasili za kutunza ngozi kavu kupita...

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa makaroni na jibini

T L