• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Raia kufungiwa nje katika mazishi ya Rais Magufuli

Raia kufungiwa nje katika mazishi ya Rais Magufuli

REHEMA MATOWO na ELIZABETH EDWARD

DAR ES SALAAM, Tanzania

WANANCHI wa kawaida hawataruhusiwa kuhudhuria misa ya mwisho na mazishi ya aliyekuwa rais wa Tanzania, hayati John Pombe Magufuli.

Wakazi wa Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita na mikoa jirani wameshauriwa kuaga mwili wa marehemu kwa kufuatilia kwenye vyombo mbalimbali vya habari vinavyorusha mubashara badala ya kwenda uwanjani.

Uamuzi huo unatokana kuwa uwanja wa Magufuli uliotengwa kwa ajili ya shughuli za kumuaga rais huyo, kuwa mdogo na hautaweza kumudu wananchi wote.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema eneo la uwanja litatumiwa na familia, viongozi wa Serikali, dini na wawakilishi wa wananchi.

Amewataka wananchi wa Mkoa wa Geita hususan wa wilaya ya Geita kujitokeza barabarani Machi 24, 2021 ili waweze kutoa heshima za mwisho, akiwataka kufanya hivyo tena Machi 25.

“Chato hapatoshi ni padogo mno niwaombe wenye changamoto, wazee, watoto na wagonjwa naomba wakae nyumbani yapo maeneo yenye runinga mnaweza kuaga kwa kuangalia mubashara. Eneo la maziko litahudhuriwa na watu wachache sana ambao ni familia na viongozi wakuu. Niwaombe sana Machi 26 ni kwa ajili ya watu wachache mno naomba mkae nyumbani mtazame runinga,” amesema Gabriel.

Kabla kufariki, Magufuli aliacha maagizo mazito ambayo alitoa mwezi Februari akiwa katika ziara zake za mwisho kukagua miradi ya maendeleo na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM.

Akiwa mkoani Morogoro mnamo Februari 11, aliwaagiza viongozi wa mkoa kushughulikia kero zilizopo katika soko jipya la Kingalu ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli bila bughudha yoyote.

Siku hiyo pia aliwataka Watanzania kuondoa hofu dhidi ya ugonjwa wa corona na kuendelea kutumia njia mbadala za kujikinga, kama kujifukizia, huku wakiendelea kuchapa kazi.

Februari 24 baada ya kuzindua daraja la juu la Kijazi na steji ya mabasi ya Magufuli, alitangaza kuvunja halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kwa sababu haina maendeleo inatekeleza na badala yake madiwani wanapokea tu fedha za kulipana posho. Jioni hiyo aliipandisha hadhi halmashauri ya Ilala kuwa jiji, kisha kumteua aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji, Spora Liana, kama mkuu wa Kinondoni.

You can share this post!

FIFA yarefusha kipindi cha marufuku kwa vinara wake za...

MAKALA MAALUM: Mzee Abae ajivunia tajriba ya kutibu nyoka...