• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
MAKALA MAALUM: Mzee Abae ajivunia tajriba ya kutibu nyoka wagonjwa kwa miaka 47

MAKALA MAALUM: Mzee Abae ajivunia tajriba ya kutibu nyoka wagonjwa kwa miaka 47

Na STEPHEN ODUOR

KWA kawaida, binadamu wengi wanapoona nyoka kinachoibuka haraka akilini ni kumuua mnyama huyo au kutoroka.

Lakini kwa mzee Bakari Abae, nyoka ni viumbe ambao wanastahili tiba wanapougua, badala ya kuuliwa kila wanapoonekana.

Abae anajivunia tajriba ya kuwatibu nyoka wagonjwa kwa miaka 47 sasa, tangu kurithi ujuzi huo kutoka kwa babake.

Mzee huyo wa miaka sabini amekuwa akivuna mapato makubwa kutokana na ujuzi wake wa kitamaduni, ambao mbali na kumpa riziki ya kila siku pia umemjengea jina na kumtembeza ulimwenguni.

Katika kijiji cha Baomo, Kaunti ya Tana River, nakutana naye akiwa ametoka kuwapa dawa nyoka wawili katika chumba cha “wagonjwa”.

“Huyu mmoja alikuwa na matatizo ya tumbo na alikuwa ywaelekea kufa. Naye huyu alikuwa na majeraha; aidha alipigana na mwenzake ama alinusurika kuliwa na joka lingine,” alieleza.

Kemia ya Bw Abae na wanyama watambaao wa kutisha ni ya kushangaza.

“Ikiwa nitamwona nyoka akipita hapa, kwa kumtazama tu ninaweza kukuambia ikiwa ana njaa au anaumwa.

“Ikiwa ni mgonjwa ninaangalia kutoka tumbo, pande, meno na macho ili kujua anaugua nini,” aeleza.

Mzee Abae alirithi ustadi huo kutoka kwa babake akiwa na umri wa miaka kumi na sita.

Anajua kabisa mimea yote inayoweza kutibu nyoka dhidi ya malaria, maumivu ya tumbo au yale yanayotokana na kuumwa na nyoka mwingine.

Katika pilkapilka zake ama hata kazini, hujipata akiwakamata nyoka wakiwa katika hali mahututi kisha huwachukua na kwenda nao nyumbani.

Wakiwa katika mazingira yale, huwatibu na kuwatenga kwa wodi ya nyoka ambapo huwalisha, kuwapa dawa na kuwafuatilia hadi watakapokuwa bora kabla ya kuwaachila kwenye mazingira.

Hii anasema hufanya kwa hiari wakati ambapo ameketi tu nyumbani bila mialiko.

Kabla ya kurudi kijijini alikuwa akifanya kazi Haller Park, ambapo alishughulikia na kuwatibu nyoka na mamba wagonjwa.

Anapoitwa kwenye mbuga za wanyama wa kutambaa huwa kwa shughuli za kuwahudumia nyoka hatari wanapogonjeka.

Kumtibu nyoka aina ya Swila, Abae hutoza Sh5,000, na Sh3,000 kwa nyoka aina ya chatu.

Nyoka wengine wadogo humpa kipato cha kati ya Sh800 na Sh1,200 kulingana na sumu na kimo cha nyoka yule.

“Nakutoza kulingana na gharama ya matibabu. Huenda yale majani nitakayotumia hayapatikani karibu, ama ile mizizi ninayohitaji ni ya kutafutwa katika msitu hatari,” aliambia Taifa Leo katika mahojiano.

Mzee huyu anabainisha kuwa sababu yake kuu ya kujiajiri ilitokana na malipo kidogo aliyokuwa akipata ilhali anahatarisha maisha yake kukamata na kutibu nyoka hatari zaidi.

Mkandarasi hakuwa akiangalia hatari, lakini uzani wa nyoka.

Kumshika nyoka aina ya Black Mamba, ambayo ni moja ya wale wanaopasa kumpa kipato cha juu zaidi, ilimfaidi kwa pesa kidogo tu ikilingana na chatu.

Wakati alitaka kulipwa Sh5,000 kwa kumkamata Black Mamba au Cobra, angepata Sh1,000; ambapo kumshika chatu, ambaye ni nyoka asiye ya sumu, angepata Sh1,500.

“Nilikuwa mmojawapo wa wale walioitwa kukamata chatu katika jumba la kumbukumbu la Kisumu. Tangu wakati huo nimefuatilia ukuaji wake, nimefahamu kuwa amehamishwa kutoka Kisumu kwenda Nairobi baada ya kimo chake kuzidi nafasi ya chumba alimowekwa.”

Hivi karibuni, amekuwa kwenye mbuga nyingi za nyoka ambapo hutibu wanyama hao; huitwa hadi mara tano kila siku kutoa huduma zake.

Mzee Abae anasema japo tajriba hiyo imekumbwa na msukosuko, inalipa.

Hata hivyo, anatoa himizo kwamba mengi yanahitaji kufanywa kwa watu wenye ujuzi huo nadra.

“Zamani, nilikuwa mimi tu lakini sasa vijana hawafuatilii taaluma hiyo tena. Kila mtu anataka kutibu binadamu na mifugo, wanasahau mazingira haya yana watoto wengine pia,” asema.

Kila mwezi hupata takriban kati ya Sh45,000 na Sh60,000 ambazo hutumia kwa karo ya watoto wake na kuwekeza kwenye vitabu na utafiti wa nyoka kwa kizazi kijacho.

Pia, huwafundisha wanawe tajriba hiyo adimu, ambapo anasema wameshika kwa upesi zaidi na hata tayari wanaitumia.

“Huu ndio urithi pekee ambao ninaweza kuwapa. Ikiwa hawawezi kuelewa hii ni bora wapate kitu kutoka shuleni. Lakini nawaambia hii haitawaacha kamwe,” asisitiza.

Katika taaluma yake, Mzee Abae amekamata baadhi ya wanyama watambaao wanaotisha zaidi, ambao wameishi katika historia.

Kwa mfano, anasema aliongoza kikundi kilichomkamata mamba maarufu “Big Daddy” kutoka River Tana.

Sanamu ya mamba huyo sasa inapamba lango la mkahawa wa watoto wa Mamba Village jijini Mombasa.

Alihusika pia katika kutafuta chatu maarufu Omieri, aliyeaga kutokana na madhara ya moto, kwenye msitu.

Mwanawe, Komora Mohammed, ameamua kuzamia ujuzi wa babake.

Kwa sasa anaweza kushughulikia Chatu na Cobra wa aina mbalimbali.

Kijana huyo bado hajaelewa maarifa ya kushughulikia Black Mamba, japo amekuwa akidurusu kwenye mtandao kujua zaidi ili kujipa maarifa kuhusu mimea ya kitamaduni ya kuwatibu nyoka na pia kutibu watu wanaoumwa na nyoka.

“Natamani serikali ingeanzisha taasisi ya tiba ya wanyama kama hawa hapa eneo letu ili wanafunzi kama mimi wajiunge kupata mafunzo kuhusu udaktari wa nyoka na pia kufanya tafiti mbalimbali,” akasema kijana Mohammed.

Mzee Abae anatumai kuwa ustadi huo hautabaki tu katika ukoo wake.

Pia anahimiza vijana kuchangamkia ujuzi wa kutibu wanyama kitamaduni, ambao umepuuzwa ilhali ni sehemu ya mazingira asili ya Kiafrika.

You can share this post!

Raia kufungiwa nje katika mazishi ya Rais Magufuli

Matokeo ya vipimo vya corona ya Mohamed Salah na timu ya...