• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Raia sasa waelekeza hasira kwa waziri mkuu

Raia sasa waelekeza hasira kwa waziri mkuu

NA MASHIRIKA

COLOMBO, SRI LANKA

WAANDAMANAJI wanaolalamikia gharama ya juu ya maisha nchini Sri Lanka, Jumatano walielekeza hasira zao kwa waziri mkuu, baada ya Rais Gotabaya Rajapaksa kutoroka nchi hiyo.

Rais Rajapaksa, 73, alitorokea katika kisiwa jirani cha Maldives na anatarajiwa kwenda kujificha Dubai.Viongozi wa upinzani Maldives wamemtaka Rajapaksa kuondoka nchini humo mara moja.

Ndugu ya Rais Rajapaksa, Basil Rajapaksa, ambaye alikuwa waziri wa fedha pia ametoroka Sri Lanka kwa kuhofia maisha yake.

Kiongozi wa upinzani Dunya Maumoon, alimtaka rais huyo kurejea nchini kwake ili kukabiliana na ghadhabu ya raia ambao wamechoshwa na uongozi wake mbovu.

Mnamo Jumatano, maafisa wa usalama walikuwa na kibarua kigumu kutawanya waandamanaji ambao walivamia ofisi ya waziri mkuu Ranil Wickremesinghe.

Lakini maelfu ya waandamanaji walitumia nguvu kuingia ndani ya ofisi hiyo na kukalia viti na kula vyakula vilivyokuwemo.

Maafisa wa usalama walisimama nje ya ofisi ya waziri mkuu bila kufanya chochote baada ya kulemewa na waandamanaji.

Waandamanaji hao walishangilia na kusherehekea huku wakisema, ‘Ranil ni mwendawazimu!’ ‘Ranil ni mwendawazimu!’

Katika juhudi za kuzima maandamano, serikali ilifunga vituo viwili vya runinga vinavyomilikiwa na serikali.

Waziri mkuu Wickremesinghe alitangaza hali ya hatari kote nchini mara baada ya Rais Rajapaksa kutoroka.

Lakini raia walipuuza agizo hilo na kumtaka kujiuzulu kufikia jana saa saba mchana.

Saa chache baada ya ofisi yake kutekwa na waandamanaji, waziri mkuu Wickremesinghe alijitokeza kwa njia ya video akiwataka wanajeshi kutumia kila njia kudumisha hali ya utulivu.

Aliwataka waandamanaji walioingia kwa nguvu katika ofisi yake na majengo mengineyo ya serikali kuondoka na badala yake washirikiane na maafisa wa usalama.

“Hatuwezi kudharau katiba yetu. Tusiruhusu wachache kuteka nyara nchi yetu; wao ni tishio kwa demokrasia,” akasema waziri mkuu huyo kupitia video iliyorekodiwa.

Rais Rajapaksa alitoroka Sri Lanka bila kujiuzulu, hatua ambayo imeacha nchi hiyo katika njia panda.

Muda mfupi baada ya Rajapaksa kutoroka nchi, spika wa bunge alitangaza kuwa waziri mkuu Wickremesinghe ameteuliwa kuwa kaimu wa rais.

Rajapaksa alikuwa ameahidi kuwasilisha bungeni barua yake ya kujiuzulu lakini kufikia Jumatano jioni hakuwa amefanya hivyo.

Raia wa Sri Lanka wamekuwa wakiandamana kwa wiki kadhaa wakilalamikia gharama ya juu ya vyakula na ukosefu wa mafuta na dawa. Raia wa Sri Lanka wanalaumu familia ya Rajapaksa ambayo imekuwa ikitawala nchi hiyo kwa miaka mingi.

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Josephat Odipo

Wanawake 30 wafanya ujima kujiendeleza kwa mtambo wa kusaga...

T L