• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:03 PM
GWIJI WA WIKI: Josephat Odipo

GWIJI WA WIKI: Josephat Odipo

NA CHRIS ADUNGO

NDOTO ya kuwa mwanahabari ilianza kumtambalia Josephat Odipo akiwa mwanafunzi wa Darasa la Tano.

Mazoea ya kusikiliza watangazaji wazoefu redioni yalinoa kipaji chake cha ulumbi na kuinua umilisi wake wa lugha.

Walimu nao walimpa fursa nyingi za kusoma habari za matukio mbalimbali gwarideni na majukwaa hayo yakampa ujasiri wa kukisarifu Kiswahili kwa wepesi.

“Vibarua nilivyofanya baada ya masomo ya sekondari vilinielekeza zaidi katika ndoto iliyokuwa lazima niote – kuwa mwanahabari,” anasema.

Odipo alizaliwa mnamo 1978 katika kijiji cha Esibembe, Butula, Kaunti ya Busia.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Bwaliro, Butula kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Lugulu AC, Butula (1994-1997).

Mnamo 1999, alielekea Eldoret kufanya vibarua vya kupakua na kupakia mizigo kwenye malori ya kusafirisha bidhaa mjini.

Kazi hizo zilimlemea, akaamua kurejea Butula baada ya miaka miwili kujishughulisha na kilimo huku akimsaidia nyanya yake katika ufugaji wa ng’ombe.

Ingawa wajomba walimtaka awe mwalimu au mwanajeshi, aliteua kusomea uanahabari katika Chuo cha Kenya Polytechnic mnamo 2001.

Alijiendeleza baadaye kitaaluma kwa kusomea shahada ya Uanahabari na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Moi (2008-2011).

Akiwa Kenya Polytechnic, alipata fursa ya kushiriki mafunzo ya nyanjani katika shirika la Kenya News Agency (KNA) mjini Kisii na kuchangia maoni na makala mbalimbali katika magazeti ya ‘Taifa Leo’, ‘Daily Nation’ na ‘The Standard’.

Mnamo Mei 2002, milango ya heri ilijifungua na akafaulu kujiunga na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC). Tukio hilo lilimkutanisha Odipo na aliyekuwa mwanafunzi mwenzake chuoni, Muraya Kariuki, ambaye sasa ni mhariri wa habari Citizen TV.

Wakiwa KBC, walianzisha kipindi cha uchambuzi wa masuala ya siasa, ‘Transition 2002’.

Ubunifu, wepesi wa kujieleza kwa Kiswahili na upana wa uelewa wa masuala ya kisiasa ni upekee uliomfanya Odipo kuaminiwa kuwa mtayarishaji wa kipindi ‘Mwamko Mpya’ katika idhaa ya KBC baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa 2002.

Mnamo Januari 2003, Odipo aliajiriwa na runinga ya KTN na akajikuza zaidi kitaaluma kwa uelekezi wa wanahabari Emmanuel Juma, Josephat Makori, Joe Ageyo, Shaban Ulaya, Nimrod Taabu, Anne Ngugi, Swaleh Mdoe na Isabella Kituri.

Mwanahabari Josephat Odipo wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO

Ingawa hayakuwa matamanio yake kuondoka KTN, haja ya kukabiliana na changamoto mpya ilimpa msukumo wa kutua Citizen mnamo Mei 2005.

Baada ya miaka miwili ya kuwa ripota wa Radio Citizen na Citizen TV, alipanda ngazi kuwa mhariri na mtangazaji wa habari chini ya Fred Afune – mkuu wa vipindi vya redio katika kampuni ya Royal Media Services (RMS) inayomiliki vituo 14 vya redio nchini Kenya.

Upekee wa Odipo katika matumizi ya Kiswahili, utayarishaji wa habari pamoja na uwasilishaji wa taarifa anazozisoma katika awamu za ‘Dira’ na ‘Jarida’ la Radio Citizen unazidi kumkweza kitaaluma.

Kinachomtambulisha zaidi ni ubunifu wa kiwango cha juu katika kipindi ‘Mchecheto’ kinachoshirikisha mbinu za ucheshi na tashtiti kumulika sarakasi za wanasiasa na vituko vinavyozunguka maisha ya binadamu katika mazingira yao ya kawaida.

Odipo amekuwa mwandalizi na mwendeshaji wa kipindi hicho katika Radio Citizen tangu 2006.

Anamstahi sana mkewe, Bi Mary Assunta Imbuhila, anayezidi kuiwekea taaluma yake thamani na mshabaha.

“Kufaulu katika uanahabari kunahitaji mtu kuwa na nidhamu ya hali ya juu pamoja na msukumo, ari na mshawasha wa kushiriki kikamilifu mafunzo yatakayomkuza kitaaluma. Ukipata mwanya wa kufanya kazi, jitume ipasavyo na uwe na mazoea ya kukamilisha majukumu yako mapema,” anashauri.

You can share this post!

TAHARIRI: Wakenya watatoa uamuzi wa mwisho kuhusu wanasiasa...

Raia sasa waelekeza hasira kwa waziri mkuu

T L