• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Rais atimua waziri mkuu, ashuku njama kumpindua

Rais atimua waziri mkuu, ashuku njama kumpindua

NA THE EASTAFRICAN

BUJUMBURA, BURUNDI

RAIS Evariste Ndayishimiye ametimua waziri mkuu wa nchi hiyo huku akidai kuwa kuna njama ya kupindua serikali yake.

Rais Ndayishimiye alimtimua Alain Guillaume Bunyoni bila kutoa sababu.

Bunge jana liliidhinisha Gervais Ndirakobuca kuwa waziri mkuu mpya.

Wabunge 113 waliohudhuria kikao cha Jumatano asubuhi waliunga mkono pendekezo la Rais Ndayishimiye kutaka Bunyoni atimuliwe.

Ndirakobuca ndiye waziri wa sasa wa usalama na masuala ya ndani. Ni kamishna wa polisi wa zamani na pia alikuwa mkuu wa majeshi ya Burundi.

Ijumaa iliyopita, Rais Ndayishimiye alipokuwa akihutubia maafisa wa serikali mjini Gitenga, alidai kuwa kuna kundi la watu wanaopanga kupindua serikali yake.

“Mnadhani kwamba amiri jeshi anaweza kushindwa na hao watu wanaopanga kunipindua? Hao watu wanaopanga kunipindua nitawashinda katika jina la Mungu,” alisema Rais Ndayishimiye bila kufichua wanaopanga kumng’oa.

Rais Ndayishimiye alifoka baada ya video ya Waziri Mkuu Bunyoni kusambazwa mitandaoni ambapo alionekana akimshambulia kiongozi wa Burundi.

Video hiyo iliweka wazi uhasama wa kisiasa ambao umekuwepo baina ya viongozi wawili hao.

“Nataka kuwaeleza wanaodhani kwamba wana mamlaka kunyenyekea. Kuna yule niliona akidai kuwa mwenye nguvu…hapa Burundi hakutakuwa na mapinduzi tena. Wanaotakia Burundi mabaya wajiandae kushindwa,” akaonya Rais Ndayishimiye.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa uhasama baina ya Bunyoni na Rais Ndayishimiye ulisababishwa na mageuzi ya sera za serikali.

“Kuna mageuzi mengi ambayo yanaendelea kufanywa kama vile kuongeza juhudi za kupambana na ufisadi,” alisema profesa wa Chuo Kikuu cha Bujumbura aliyetaka jina lake libanwe.

Rais Ndayishimiye aliyechukua hatamu za uongozi wa taifa hilo la Afrika Mashariki mnamo Juni 2020, aliahidi kurejesha utawala wa sheria na kupambana vikali dhidi ya ufisadi.

Vita dhidi ya ufisadi vimesababisha maafisa kadhaa wa serikali kutimuliwa. Umoja wa Ulaya (EU) iliondoa vikwazo vya kiuchumi walivyoweka dhidi ya Burundi ukisema kuwa Rais Ndayishimiye amepiga hatua kubwa katika kupambana na ufisadi na kurejesha utawala wa sheria.

Burundi ilikumbwa na machafuko mnamo 2015 Rais Pierre Nkurunziza – aliyeaga dunia mnamo Juni 2020 – alipotangaza kampeni za urais kwa muhula wa tatu.

Waziri mkuu mpya Ndirakobuca aliwekewa vikwazo na Amerika mnamo 2015 kutokana na juhudi zake za ‘kunyamazisha’ waliokuwa wakipinga hatua ya Nkurunziza kuwania muhula wa tatu.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge na maseneta waapishwa kuanza majukumu yao

GWIJI WA WIKI: Suleiman Fadhili

T L