• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Rubani asifiwa kwa kuzuia ajali licha ya mshtuko wa nyoka

Rubani asifiwa kwa kuzuia ajali licha ya mshtuko wa nyoka

Na AFP

JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI

RUBANI wa ndege moja iliyotua ghafla ila salama, baada ya kushtuliwa na nyoka jana alimiminiwa sifa kwa “kitendo hicho cha ujasiri wa kipekee.”

Rudolf Erasmus alikuwa akiendesha ndege ndogo yenye abiria wanne kutoka Blomfontein hadi Pretoria wiki hii alipohisi nyoka aina ya swila akipitia mgongoni mwake.

Licha ya kupatwa na mshtuko, alidhibiti ndege hiyo na ikatua salama katika mji wa Welkom, ulioko katikati ya miji mikubwa ya Bloemfontein na Pretoria.

“Ningependa kumpongeza Rudolf kwa hatua ya kijasiri aliyochukua na jinsi alivyodhibiti hali ambayo ingesababisha ajali kubwa ya ndege,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Angani Afrika Kusini (SACAA) Poppy Khoza.

“Alisalia mtulivu katika hali hatari na akaiwezesha ndege hiyo kutua salama bila yeye au abiria wake kuumia. Alidhihirishia ulimwengu kwamba yeye ni balozi mkuu wa usalama wa safari za angani,” Bw Khoza akaongeza.

Ijumaa, Erasmus aliwaambia wanahabari kwamba aligundua uwepo wa nyoka huyo akiwa safarini baada ya kuhisi kitu baridi kikigusa mgongo wake.

“Mwanzoni nilidhani ilikuwa ni chupa yangu ya maji… lakini baadaye niligundua kuwa kilikuwa kitu kingine na hivyo sikusonga,” akawaambia wanahabari.

Kisa hicho kilitokea mnamo Jumatano wiki hii.

Nyoka aina ya swila hupatikana kwa wingi kusini magharibi ya Afrika Kusini. Nyoka hao ni hatari kwa sababu wanayo sumu kali ambayo huhitaji tiba ya haraka wakimuuma binadamu.

  • Tags

You can share this post!

Handiboli: Handege yalipua Mang’u High

Karua amkejeli Ruto kwa kuzindua mradi mara mbili

T L