• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Rwanda yakemea DRC vita vikinukia

Rwanda yakemea DRC vita vikinukia

NA PATRICK ILUNGA

KINSHASA, DRC

JESHI la Ulinzi la Rwanda (RDF) limeshutumu wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) kwa kurusha roketi ndani ya Rwanda Ijumaa huku mapigano yakianza tena kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa DRC katika eneo la Rutshuru.

Watoto wawili waliuawa katika mapigano hayo.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari, RDF inasema kuwa wanajeshi wa FARDC walifyatua roketi mbili ndani ya Rwanda kutoka eneo la Bunagana.

Roketi hizo zilianguka katika eneo la Cellule Nyabigoma, wilaya ya Muzanze mnamo Juni 10 mwendo wa saa tano na dakika 55 mchana.

Hakuna majeruhi yaliyoripotiwa lakini wakazi wa eneo hilo karibu na mpaka wa Rwanda na DRC wamejawa na hofu kuhusu usalama wao kufuatia tukio hilo.

Wanajeshi wa Rwanda waliongeza kuwa wanajeshi wa DRC walirusha makombora mengine ndani ya himaya ya nchi hiyo mnamo Mei 19 na Mei 23 na kuwajeruhi idadi isiyojulikana ya watu kando na kuharibu mali.

RDF inasema kuwa Serikali ya DRC ilifahamishwa kuhusu mashambulio hayo pamoja na shirika la kufuatilia usalama katika Eneo la Maziwa Makuu na washirika wengine.

Rwanda imetisha kulipiza kisasa endapo wanajeshi wa DRC wataendelea na mashambulizi dhidi ya nchi hiyo.

Lakini kulingana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni Christopher Lutundula mnamo Mei 25 jeshi la Rwanda lilirusha makombora na mabomu 20 katika eneo la Katale, kama hatua ya kulipiza kisasi.

Mabomu hayo yaliangushwa karibu na uwanja wa ndege unaomilikiwa na chuo cha Congolese Institute for Nature Conservation karibu na mji wa Rumangabo ulioko Kivu Kaskazini.

DRC na Rwanda yanakaribia kuanza vita vikali pamoja na kuvunjika kwa uhusiano wa kidiplomasia kati yao.

Kila moja ya nchi hizo inashutumu mwenzake kwa madai ya kuunga mkono makundi ya waasi yanayolaumiwa kutekeleza mauaji na uharibifu wa mali.

Kupitia taarifa mnamo Juni 8, majeshi ya DRC yalidai kuwa Rwanda imewatuma wanajeshi wake 500 kuunga mkono waasi wa M23. Rwanda ilikana madai hayo.

Mchakato wa kupatanisha mataifa hayo mawili umeanza na unaongozwa na Rais wa Angola João Lourenço.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Ruto, Raila wachezea Wakenya karata hatari...

JUNGU KUU: Wawaniaji wa ODM Nyanza hawapumui

T L