• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
JUNGU KUU: Wawaniaji wa ODM Nyanza hawapumui

JUNGU KUU: Wawaniaji wa ODM Nyanza hawapumui

NA CHARLES WASONGA

WAWANIAJI wa viti mbalimbali, hasa ugavana, kwa tiketi ya ODM kati eneo la Nyanza watalazimika kujikaza kisabuni kushinda viti hivyo katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Hii ni baada ya jopo linalosimamia kampeni za mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga kutangaza kuwa wawaniaji wa vyama vingine katika muungano huo wako huru kushindana na wa ODM, kwa usawa.

Mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi, ambaye ni mwanachama wa jopo hilo, amesema uamuzi huo umefikiwa kwa lengo la kuhakikisha wakazi wanajitokeza kwa wingi kumpigia kura Bw Odinga.

“Sasa tuko ndani ya Azimio na hatuwezi kuwapigia debe wagombeaji wa ODM pekee. Tunawahitaji wenzetu kutoka vyama vingine pia katika kaunti nyingine zote za Nyanza ili wavutie kura za urais katika debe la Raila. Lengo letu kuu ni kutwaa kiti cha urais,” akasema kwenye kikao na wanahabari Kisumu mnamo Ijumaa wiki jana.

Hata hivyo, Bw Mbadi, ambaye ni mbunge wa Suba Kusini anayeondoka, alisisitiza kuwa wagombeaji viti mbalimbali hawatapigiwa debe hadharani katika mikutano ya kampeni itakayoongozwa na Bw Odinga katika eneo pana Nyanza.

“Ushauri wangu kwa wagombeaji wa ODM ni kwamba wanafaa kujipanga upya na wakubali kuendesha kampeni pamoja na wenzao kutoka vyama vingine vilivyo ndani ya Azimio. Hii ni kwa sababu vyama hivi vyote vinaunga mkono Raila katika kinyang’anyiro cha urais,” akaongeza.

Hata hivyo, Bw Mbadi alidinda kutoa msimamo wowote kuhusu iwapo Azimio inawakubali wagombeaji wa kujisimamia au la.

Kauli hiyo ya Mbadi inajiri huku Bw Odinga akitarajiwa kuzuru Kaunti ya Kisii leo Jumatatu, kuendesha kampeni ya kuwarai wakazi wampigie kura za urais.

Baadaye atatembelea kaunti za Nyamira, Migori, Homa Bay, Siaya na hatimaye kukamilisha ziara katika Kaunti ya Kisumu.

Bw Odinga analenga kukinga sehemu kubwa ya jumla ya kura milioni 2.7 za eneo hilo la Nyanza, zisitwaliwe na mpinzani wake mkuu Naibu Rais William Ruto.

Katika Kaunti ya Kisii, mgombea ugavana kwa tikiti ya ODM, Bw Simba Arati anakabiliwa na upinzani kutoka kwa Seneta wa sasa Sam Ongeri anayewania kwa tiketi ya DAP-K na aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Uchukuzi, Chris Obure wa chama cha Jubilee.

Watatu hao ambao vyama vyao vina washirika ndani ya muungano wa Azimio wanapambana wao kwa wao, pamoja na mgombezi wa kiti hicho kwa chama cha UDA, mbunge wa Nyaribari Masaba, Ezekiel Machogu.

Japo Kisii inasawiriwa kama ngome ya ODM, itabidi Bw Odinga kuwakumbatia Prof Ongeri na Bw Obure mbali na Bw Arati ambaye ni mbunge anayeondoka wa Dagoretti Kaskazini.

Hii ni kwa sababu, kulingana mtazamo wa Bw Mbadi, wafuasi wa vyama vya Jubilee na DAP-K wanafaa kuhisi kuthaminiwa ndani ya Azimio.

Kinyang’anyiro kikali kati ya vyama tanzu vya Azimio pia kinatarajiwa kushuhudiwa katika kaunti jirani ya Nyamira.

Mweka Hazina wa Kitaifa wa ODM, Timothy Bosire anashindana na gavana wa sasa Amos Nyaribo anayetetea kiti chake kwa tiketi ya UPA, na Mbunge wa Borabu Ben Momanyi wa chama cha Wiper.

Katika Kaunti ya Migori, kivumbi kitashuhudiwa katika kinyang’anyiro cha kiti cha ugavana kati ya Seneta Ochilo Ayacko wa ODM, waziri wa zamani Dalmas Otieno (Jubilee) na aliyekuwa Mbunge wa Migori, John Dache Pesa (DAP-K).

Lakini huenda mgombeaji wa ugavana wa Homa Bay, Gladys Wanga (ODM) akafaidi kutokana na kampeni za Bw Odinga katika eneo hilo kwani vyama vingine katika Azimio havijadhamini wagombeaji.

Mpinzani mkuu wa Bi Wanga ni aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Evans Kidero anayewania kiti hicho kama mgombeaji wa kijitegemea.

Duru zinasema Dkt Kidero anamtoa kijasho Bi Wanga, na italazimu ODM kuongeza kasi ya kampeni ili ishinde kiti hicho.

Naye Gavana wa Kisumu, Prof Anyang Nyong’o anayetetea kiti chake kwa tikiti ya ODM anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa gavana wa zamani Jack Ranguma anayewania kwa MDG.

Chama hicho, kinachoongozwa na Mbunge wa Ugenya, Bw David Ochieng, pia ni mojawapo ya jumla ya vyama 26 katika muungano wa Azimio.

Aidha, chama hicho pia kimemdhamini Mbunge wa Kisumu Mjini Magharibi, Bw John Olago Aluoch kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa Agosti.

Bw Aluoch, anayepania kuhudumu kwa muhula wa tatu kama mbunge wa eneo hilo atapambana na Bi Rosa Buyu anayeng’ang’ania kiti hicho kwa tikiti ya ODM.

Katika Kaunti ya Siaya, Seneta James Orengo ambaye anawania useneta kwa tikiti ya ODM amekabwa koo na aliyekuwa Mbunge wa Rarieda, Bw Nicholas Gumbo anayewania kwa UDM.

Chama hicho kinaongozwa na Gavana wa Mandera, Ali Roba, aliye msimamizi wa kampeni za Bw Odinga katika kaunti hiyo.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anapongeza hatua ya kuruhusu vyama tanzu vya Azimio kushindania viti mbalimbali katika ngome zake akisema hatua hiyo itachangia idadi kubwa ya wapigakura kujitokeza.

“Hata hivyo, muungano huo uwe makini zaidi katika utekelezaji wa mpango huo usije ukapoteza viti katika maeneo ambako mrengo pinzani wa Kenya Kwanza una wawaniaji wenye ushawishi mkubwa.”

  • Tags

You can share this post!

Rwanda yakemea DRC vita vikinukia

Tatizo la digrii lawakosesha Samboja na Sakaja usingizi

T L