• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
Takriban raia wa Uganda 46 hufariki kwa Ukimwi kila siku

Takriban raia wa Uganda 46 hufariki kwa Ukimwi kila siku

NA MASHIRIKA

KAMPALA, UGANDA

WIZARA ya afya nchini Uganda imesema raia wa Uganda 46 hufariki kila siku kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Kufuatia tangazo hilo, bunge limeiomba serikali kuanzisha upya kampeni kali za uhamasisho kuhusu ukimwi.

Isitoshe, wabunge wamesisitiza, hamasisho lifanyike haswa miongoni mwa vijana ili kupunguza kasi ya maambukizi. Wito huo ulifuatia taarifa ya Waziri wa Urais, Bi Milly Babalanda, iliyoangazia kiwango cha juu cha maambukizi kati ya vijana.

“Maambukizi kati ya vijana wa miaka 15-24 yalichangia asilimia 37 ya maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi mwaka 2021. Maambukizi mapya yakitokea mara tatu zaidi kati ya wasichana wadogo ikilinganishwa na wavulana katika kipindi hicho,” Bi Balalanda akasema.

Bi Balalanda alisema hayo alipokuwa akinukuu takwimu kutoka kwa Wizara ya Afya.

Alisisitiza zaidi kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, nchi bado inakabiliwa na changamoto nyingi.

“Takriban watu 1,000 huambukizwa virusi vya Ukimwi kila wiki na takriban watu 325 hufa kila wiki kutokana na vifo vinavyohusiana na Ukimwi,” alisema.

Mwakilishi wa Wanawake eneo na Rakai, Bi Juliet Kinyamatama, alisema maambukizi mapya ni mengi miongoni mwa rika la kwenda shule.

“Ofisi ya Rais na Wizara ya Elimu wanapaswa kufanya kazi pamoja ili kuona kwamba tuna kampeni za shule,” alisema.

Mbunge wa Kike katika eneo la Gulu, Bi Betty Aol Ochan, alisema awali, watu wote walikuwa makini kwa kutahadhari na masuala yanayohusiana na Ukimwi kuliko siku hizi.

“Katika miaka ya hapo nyuma, kila mtu alikuwa macho. Tulipigana na virusi na kupunguza visa lakini sasa kila kitu kiko kimya, kana kwamba tumeridhika. Vijana wanadhani ukimwi ni kama malaria au mafua,” Bi Ochan akaongeza

Waziri huyo aliongeza kuwa maambukizi mapya yanachochewa na, miongoni mwa mengine, ngono ya kiholela, dhulma za kijinsia na ndoa za mapema.

Vilevile, ngono ya miamala, utofauti wa mapato na umaskini; kiwango cha juu cha kuacha shule; unyanyapaa na ubaguzi na huduma za utunzaji na matibabu.

Kadhalika, kutokana na watu kufungiwa kufuatia janga la Corona miaka miwili iliyopita pia kulipuuza juhudi za kudhibiti janga hilo ikiwa ni pamoja na kutatiza huduma za kufikia vituo vya kuhudumia waathiriwa.

Kuna watu milioni 1.4 wanaoishi na virusi vya ukimwi nchini Uganda.

  • Tags

You can share this post!

KINYUA KING’ORI: Vikao vya Raila kutetea makamishna...

GWIJI WA WIKI: DJ Kezz

T L