• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 2:24 PM
Tetemeko: Watu 2,012 wathibitishwa kufariki nchini Morocco

Tetemeko: Watu 2,012 wathibitishwa kufariki nchini Morocco

NA MASHIRIKA

MARRAKESH, MOROCCO

KUFIKIA Jumapili, Septemba 10, 2023, saa kumi na mbili jioni, watu 2,012 walikuwa wamethibitishwa kuaga dunia kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea nchini Morocco mnamo Ijumaa, kulingana na Wizara ya Masuala ya Ndani ya nchi hiyo.

Kwenye taarifa wizara hiyo iliongeza kuwa kufikia wakati huo idadi ya waliojeruhiwa ilikuwa imefika 2,059, huku watu 1,404 wakiwa hali mahututi.

Kufuatia mkasa huo uliotokea katika eneo la milima umbali wa kilomita 72 kusini mwa mji wa kali wa Marrakesh, serikali ya Morroco imetangaza siku tatu za kitaifa za maombolezo.

Ndani ya kipindi hicho, bendera zote za kitaifa nchini humo zitapeperushwa nusu mlingoti kwa heshima ya waliokufa.

Jeshi la Morocco limebuni makundi ya maafisa wa kuendesha shughuli za uokoaji na kutoa misaada ya kimsingi kwa manusura wa mkasa huo wa kihistoria.

Makundi hayo yanasambaza aina mbalimbali za misaada kama maji safi ya kunywa, chakula, huma, dawa, blanketi miongoni mwa mahitaji mengine ya kimsingi.

Aidha, nchi kadha zikiwemo Israel, Ufaransa, Uhispania, Italia, Amerika miongoni mwa nyingine zimetoa aina mbalimbali za msaada kwa serikali ya Morocco wakati huu mgumu.

Hata nchi jirani ya Algeria, licha ya kuwa na uhasama wa kidiplomasia na Morocco, imefungua anga yake kuruhusu ndege za kusafirishia ili kufikisha misaada Morocco. Aidha, taifa hili limetoa aina mbalimbali za misaada kwa makundi yanayoendelesha shughuli za uokoaji na kusaka manusura zaidi.

Shirika la Msalaba Mwekundu linasema kuwa itachukua muda mrefu na wenye changamoto kabla ya hali ya kawaida kurejea nchini Morocco haswa katika kitovu cha tetemeko hilo na maeneo ya karibu.

“Shughuli ya kukarabati uharibifu uliosababishwa na tetemeko hilo huenda zikachukua miezi na hata miaka,” shirika hilo likasema kwenye taarifa Jumapili.

Maeneo yaliyoathirika zaidi yanajumuisha mkoa wa Al-Haouz, kitovu cha tetemeko hili, ambako watu 1,293 wamethibitishwa kufa. Linafuatwa na mkoa wa Taroudant ambako watu 452 wameripotiwa kupoteza maisha.

  • Tags

You can share this post!

Betty Maina wa Murang’a ashauriwa adhibiti ulimi wake

LATA: Kundi la wasanii linalosaidia waraibu kuachana na...

T L