• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Tutanasa magari yote ya serikali, Chebukati aonya wagombea

Tutanasa magari yote ya serikali, Chebukati aonya wagombea

NA LEONARD ONYANGO

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeagiza kukamatwa kwa magari na mali ya serikali inayotumiwa na wanasiasa katika kampeni.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati ametoa makataa ya siku 14 kwa magavana, manaibu gavana, wabunge, madiwani na watumishi wengineo wa umma kupeleka katika makao makuu ya tume hiyo jijini Nairobi orodha ya mali ya serikali ambayo wamekuwa wakitumia katika utekelezaji wa majukumu yao.

Bw Chebukati alionya kuwa wanasiasa watakaokosa kufanya hivyo kufikia Juni 10, 2022, watachukuliwa hatua kali ya kisheria.

Kifungu cha 14 (1) cha Sheria kuhusu Makosa ya Uchaguzi, kinapiga marufuku wanasisa kutumia rasilimali za umma katika kampeni.

Magari ni miongoni mwa mali ya serikali ambayo imekuwa ikitumiwa na wanasiasa kupiga kampeni.

Jumanne, polisi walinasa gari linalomilikiwa na ofisi ya Hazina ya Ustawishaji wa Maeneobunge (NG-CDF) likiwa limepakwa rangi nyingine na kuwekewa picha za mbunge wa Kimilili Didmus Barasa na Naibu wa Rais William Ruto.

Kulingana na polisi, Bw Barasa alikuwa ameliwekea nambari feki za usajili: KBS 709D badala ya GK948J.

Baadaye, mbunge huyo hakukamatwa ila alijitokeza na kuwataka wamkamate kwanza kinara wa Azimio Raila Odinga – aliyedai anatumia magari ya serikali – kabla ya kumkamata yeye.

Bw Chebukati alisema Ijumaa kuwa mali ya umma, yakiwemo magari, itakayopatikana ikitumiwa katika kampeni itanaswa na wahusika watatozwa faini ya Sh2 milioni au kuhukumiwa kifungo cha miaka isiyozidi sita gerezani.

“Tume ya IEBC ina mamlaka ya kuagiza kunaswa kwa mali ya umma itakayopatikana katika misafara ya kampeni,” akasema Bw Chebukati.

Sheria hiyo imeacha nje Naibu wa Rais Ruto na mawaziri ambao wamekuwa wakishutumiwa kwa kutumia rasilimali za umma kama vile magari na mafuta katika kampeni.

Kambi ya Dkt Ruto imekuwa ikishutumu mawaziri Fred Matiang’i (Usalama) na Joe Mucheru (Teknolojia ya Mawasiliano) kwa kutumia rasilimali za umma kusaidia Bw Odinga.

Kifungu cha 23 cha Sheria kuhusu Uongozi na Maadili kinaruhusu mawaziri pamoja na makatibu wa wizara kujihusisha na siasa licha ya kuwa watumishi wa umma.

“Magavana, manaibu gavana, wabunge, madiwani, maafisa wa mashirika ya serikali wanaowania viti vya kisiasa ni sharti walete orodha ya rasilimali zote za serikali ambazo wamekuwa wakitumia kutekeleza majukumu yao rasmi. Orodha hiyo iwasilishwe ndani ya siku 14 katika Jumba la Anniversary Towers jijini Nairobi,” akasema Bw Chebukati.

  • Tags

You can share this post!

EACC yaandama Sh1.9 bilioni za Waititu

Liverpool vs Real Madrid: Leo ni leo!

T L